Ka´b al-Ahbar amesema:

”Allaah amesema ndani ya Tawraat: ”Mimi ni Allaah juu ya waja wangu na ´Arshi Yangu iko juu ya viumbe vyangu vyote. Nami niko juu ya ´Arshi Yangu na ninasimamia mambo ya waja Wangu. Hakuna kilichojificha Kwangu katika mbingu wala ardhini.”[1]

Ameipokea Abush-Shaykh, Ibn Battwah na wengineo.

al-Hasan al-Baswriy amesema:

”Yuunus (´alayhis-Salaam) alisikia matakaso ya kokoto na samaki ambapo akaanza kusabihi. Alikuwa akisema katika du´aa yake: ”Ee Mola wangu, makazi Yako yako juu mbinguni na uwezo Wako uko ardhini… ”[2]

Ameipokea Imaam Muwaffaq-ud-Diyn i ”Ithbaatu Swifat-il-´Uluww”.

Abu Bakr al-Hudhaliy amepokea ya kwamba al-Hasan amesema:

”Hakuna chochote kilicho karibu zaidi na Mola wako kuliko Israafiyl. Baina yake na baina Yake kuna mapazia saba. Kila pazia ni sawa na miaka mia tano. Chini yake yupo Israafiyl. Kichwa chake kiko chini ya ´Arshi na miguu yake iko chini ya ardhi ya saba.”[3]

Imethibiti kutoka kwa Masruuq kwamba alikuwa akihadithia kutoka kwa ´Aaishah husema:

”Amenihadithia mwanamke mkweli, msichana wa mwanaume mkweli, mpenzi wa mpenzi wa Allaah, mwanamke aliyetakaswa kutoka juu ya mbingu ya saba.”[4]

Ibn ´Abbaas aliingia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) wakati alipokuwa katika hali ya kukata roho akamwambia:

”Wewe ulikuwa ndiye mwanamke unayependeza zaidi mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – na hakuwa akipenda isipokuwa vilivyo vizuri tu. Allaah amekutakasa kutoka juu ya mbingu saba.”[5]

Qataadah amesema:

”Wana wa israaiyl walikuwa wakisema: ”Ee Mola! Wewe uko juu ya mbingu na sisi tuko ardhini. Ni vipi tutajua radhi Zako kutokana na dhahabu Zako?” Akasema: ”Ninapokuwa radhi nanyi basi hukutawalishieni wabora wenu, na ninapokuwa nimewakasirikieni huwatawalishieni waovu wenu.”[6]

Ameipokea ad-Daarimiy.

Thaabit al-Bunaaniy amesimulia:

”Daawuud alikuwa akirefusha swalah, kisha akirukuu, kisha akinyanyua kichwa chake kuelekea mbinguni na akisema: ”Wewe Uliye juu ya mbingu! Nimekiinua kichwa changu kukielekeza Kwako, kama ambavo watumwa wanawatazama mabwana zao, ee Ambaye unaishi juu ya mbingu!”[7]

Ameipokea al-Laalakaa´iy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Maalik bin Diynaar amesema:

”Chukua na usome. Sikiliza maneno ya Mkweli kutoka juu ya ´Arshi Yake.”[8]

Ameipokea Abu Nu´aym katika ”Hilyat-ul-Awliyaa’” kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

adh-Dwahhaak amesema kuhusiana na maneno Yake (Ta´ala):

مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَىٰ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا

“Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao, na wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao, na wala chini kuliko ya hivyo na wala wengi zaidi isipokuwa Yeye yupamoja nao popote watakapokuwa, kisha siku ya Qiyaamah atawajulisha yale waliyoyatenda; hakika Allaah juu ya kila jambo ni mjuzi.”

”Yupo juu ya ´Arshi Yake na ujuzi Wake uko pamoja nao.”[9]

Ameipokea Ibn ´Abdil-Barr na wengineo.

[1] Wasimulizi wake ni wenye kuaminika kwa mujibu wa adh-Dhahabiy katika ”al-´Uluww”, uk. 121. Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa Ibn-ul-Qayyim katika ”Ijtimaa´-ul-Juyuush al-Islaamiyyah”, uk. 102.

[2] adh-Dhahabiy amesema kwamba ”Ishaaq bin Bishr alikuwa dhaifu na aliyeharibika” (Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (9/478).

[3] adh-Dhahabiy amesema kwamba ”Abu Bakr al-Hudhaliy ni dhaifu mno” (al-´Uluww, uk. 93).

[4] Swahiyh kwa mujibu wa adh-Dhahabiy katika “al-´Uluww” na Ibn-ul-Qayyim katika “Ijtimaa´-ul-Juyuush al-Islaamiyyah”, uk. 102.

[5] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh yenye masharti ya Muslim kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Mukhtaswar-ul-´Uluww” (106).

[6] Imethibiti kutoka kwa Qataadah kwa mujibu wa adh-Dhahabiy katika ”al-´Uluww”, uk. 126, cheni ya wapokezi ni nzuri kwa mujibu wa  al-Albaaniy katika “Mukhtaswar-ul-´Uluww” (107).

[7] Cheni yake ya wapokezi iko salama kwa mujibu wa adh-Dhahabiy katika ”al-´Uluww”, uk. 67.

[8] Hilyat-ul-Awliyaa’ (2/358). Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa adh-Dhahabiy katika “al-´Uluww”, uk. 128, na Ibn-ul-Qayyim katika “Ijtimaa´-ul-Juyuush al-Islaamiyyah”, uk. 102.

[9] Jaamiy´-ul-Bayaan (23/237) ya at-Twabariy, as-Sunnah (592) ya ´Abdullaah bin Ahmad bin Hanbal na al-Asmaa’ was-Swifaat” (430) ya al-Bayhaqiy. Cheni ya wapokezi ni nzuri kwa mujibu wa adh-Dhahabiy katika “al-´Uluww”, uk. 129.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad bin ´Abdil-Haadiy al-Maqdisiy (afk. 744)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Kalaam ´alaa Mas-alat-il-Istiwaa’ ´alaal-´Arsh, uk. 44-48
  • Imechapishwa: 21/12/2025