09. Kuzikusanya tafsiri zote za Salaf ni muhimu sana

Maelezo yote ya Salaf kuhusu masuala kama haya ni jambo lenye manufaa sana. Hii ni kwa sababu mkusanyiko wa maelezo yao yote unaonyesha vyema zaidi makusudio kuliko maelezo moja au mawili. Hata hivyo lazima kuwepo na tofauti za msingi miongoni mwao, kama vile zinavyopatikana tofauti katika hukumu mbalimbali za Kishari´ah. Tunajua kwamba masuala mengi ambayo wengi miongoni mwa watu wamekhitilafiana yanatambulika vyema kwa wote – bali yamepokelewa kwa mapokezi mengi kwa watu wa kawaida na wanazuoni. Hii ni kama idadi ya Rak´ah za swalah, kiwango chake na nyakati zake, ufaradhi wa zakaah na viwango vyake, kuilengesha Ramadhaan, Twawaaf, kusimama ´Arafah, kurusha vijiwe kwenye Nguzo, vituo na kadhalika. Tofauti za maoni miongoni mwa Maswahabah, kama kuhusu masuala ya urithi kati ya babu na ndugu wa aliyekufa, urithi wa ndugu, kushirikiana katika urithi na mfano wake hazisababishi shaka yoyote katika masuala ya msingi ya mirathi. Allaah ameteremsha Aayah tatu zinazofafanua masuala ya mirathi ambazo watu wengi wanahitaji, ikiwa ni pamoja na mirathi ya wazazi, mirathi ya watoto, mirathi ya ndugu wasio na watoto na mirathi ya wanandoa. Katika ya kwanza Amewataja wazazi na vizazi vyao, katika ya pili Ametaja warithi wanaorithi urithi uliowekwa na ya tatu Ametaja warithi wasiorithi urithi uliowekwa, nao ni wale ndugu wa baba na mama tumbo moja au wale wa baba pekee. Ni mara chache babu na ndugu wote kuwa hai wakati mwosia anapokufa. Kwa ajili hiyo jambo hilo halikutokea katika Uislamu isipokuwa baada ya kufariki kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Tofauti za maoni zinaweza kujitokeza kwa sababu ya udhaifu wa dalili. Zinaweza kujitokeza kwa sababu watu hawakuzisikia. Sababu nyingine ni kuifahamu kimakosa. Kwa kuongeza inaweza kutokana na kuamini kwamba kuna hoja yenye nguvu inayopingana. Madhumuni hapa ni kufafanua maelezo ya jumla ya jambo hili pasi na kuingia kwenye maelezo ya kina.

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 46-47
  • Imechapishwa: 31/03/2025