60 – Kwa njia hiyohiyo ametuhadithia Sulaymaan bin Harb, kutoka kwa Hammaad bin Zayd, ambaye amesema:

”Ayyuub alinikabidhi nguo akasema: “Nikatie iwe kama kanzu. Uweke sehemu ya mwisho ya mkono wake kuwa shibri na uifanye iingie hadi juu ya kisigino.”

61 – Ishaaq bin Ibraahiym ametuhadithia, kutoka kwa ´Abdur-Razzaaq, kutoka kwa Ma´mar, ambaye amesema:

”Nilimkosoa Ayyuub juu ya urefu wa kanzu yake, akasema: “Hakika umaarufu zamani ulikuwa katika urefu wake, lakini leo ni katika kuikunja.”

62 – Muhammad bin Sallaam al-Jumahiy ametuhadithia: ´Adiy bin al-Fadhwl ametuhadithia: Ayyuub amenambia:

“Tengeneza viatu viwili kwa namna ya mfano wa viatu vya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Nikafanya hivyo. Akavivaa kwa siku kadhaa kisha akaviacha. Nikamuuliza kuhusu hilo, akasema: “Sikuona watu wakivivaa.”

63 – ´Aliy bin al-Ja´d ametuhadithia: Qays bin ar-Rabiy´ ametukhabarisha, kutoka kwa Mansuur, kutoka kwa Ibraahiym, ambaye amesema:

“Usivae katika nguo kile ambacho wanavyuoni watakujua kwa sababu yake wala wajinga wakakudharau kwa sababu yake.”

64 – al-Hakam bin Muusa ametuhadithia: Ghassaan bin ´Ubayd ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan ath-Thawriy, ambaye amesema:

“Walikuwa wanachukia aina mbili za umaarufu: nguo nzuri sana ambazo mtu anajulikana nazo na watu wanainua macho yao kumwangalia kwa sababu yake, na nguo mbaya sana ambazo mtu anadharauliwa na dini yake kudhalilishwa.”

65 – Khaalid bin Khidaash ametuhadithia: Hammaad bin Zayd ametuhadithia, kutoka kwa Abu Khushaynah, swahiba yake az-Ziyaadiy, aliyesema:

”Siku moja tulikuwa pamoja na Abu Qilaabah wakati alipoingia bwana mmoja ambaye alikuwa amevaa mashuka. Akasema: “Jihadharini na huyu punda mpiga kelele.”

66 – Khalaf bin Hishaam ametuhadithia: Hammaad bin Zayd ametuhadithia, kutoka kwa bwana mmoja, kutoka kwa Abu Bakr, kutoka kwa al-Hasan, ambaye amesema:

“Hakika kuna watu ambao wamefanya kiburi kuwa katika mioyo yao na unyenyekevu katika nguo zao. Hivyo basi mwenye joho la kawaida amejivuna zaidi kuliko mwenye joho la kifakhari – muda wa kuwa hawajifanyi kuwa ni mafukara.”

67 – Abu Ishaaq Ismaa´iyl bin al-Haarith ametuhadithia:: Muhammad bin Muqaatil ametuhadithia: Ibn-ul-Mubaarak ametuhadithia: Abu ´Awaanah ametuhadithia, kutoka kwa Sulaymaan ash-Shaybaaniy: Bwana mmoja ametuhadithia:

”Ibn ´Umar alimuona mwanawe amevaa kanzu mbaya na ya hali ya chini, akasema: “Usivae hii. Hakika hii ni kanzu ya umaarufu.”

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa (afk. 281)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Khumuul wat-Tawaadhwu´, uk. 84-91
  • Imechapishwa: 29/01/2026