09. Huyu ndiye maiti ambaye inalazimika kumfungia

Tambua ya kwamba makusudio ya Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ni pale ambapo mgonjwa ataweza kufunga swawm ambayo inamlazimu kwa njia ya kwamba amepona kutoka katika maradhi yake au ndio punde ametoka katika safari yake na hakuwahi kufunga mpaka akafariki, kwa vile ni swawm inayomlazimu, basi atalipiwa nayo kama anavyolipiwa deni. Lakini ikiwa hakuweza kulipa kwa njia ya kwamba yakaendelea maradhi, hedhi ikaendelea, damu ya uzazi ikaendelea mpaka kifo kikamkuta au akabaki huko ugenini mpaka akafariki, huyu hatolipiwa na wala warithi wake hawahitaji kulisha chakula kwa mujibu wa maoni ya kikosi cha wanazuoni wengi. Imemdondokea kwa kutoweza kwake kulipa.

Jamaa zake wasipoweza kumfungia maiti basi kutatolewa chakula kutoka katika mirathi yake kuwalisha masikini kwa kila siku aliyoiacha. Kila masikini atapewa Mudd ya ngano nzuri. Kiwango cha Mudd ni gramu 563. Inafaa pia kwa walii wake kuwakusanya masikini akawashibisha kwa idadi ya siku ambazo maiti anadaiwa. Hilo ni kutokana na yale yaliyopokelewa kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh):

“Kwamba kuna mwaka alidhoofika kufunga ambapo akatengeneza bakuli la Thariyd na akawaalika masikini thelathini na akawashibisha.”[1]

Itasihi pia endapo hatokuwa na warithi ambapo akajitolea mtu kulishiza chakula kwa niaba yake. Asipojitolea yeyote basi jambo lake anaachiwa Allaah (Ta´ala). Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Ee Allaah! Tufishe tukiwa waislamu, tuunganishe na waja wema pasi na fedheha wala wenye kupewa mtihani. Ee Allaah! Tusamehe madhambi yetu, zisitiri aibu zetu, ijaalie swawm yetu ni yenye kukubaliwa, thawabu za matendo yetu kuwa nyingi kwa rehema Zako, ee Mwingi wa huruma kuliko wenye kurehemu wote.

[1] ´Abdur-Razzaaq (7570), Ibn Abiy Shaybah (07/533), ad-Daaraqutwniy (02/207) na wengineo. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh na iliyothibiti. Tazama “Sharh-ul-´Umdah” Kitaab-us-Swiyaam (02/260).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 94-95
  • Imechapishwa: 16/03/2023