09. Hadiyth “Yeyote atakayehiji na asitamke maneno ya matusi wala kufanya ufuska… ”

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Yeyote atakayehiji na asitamke maneno ya matusi wala kufanya ufuska, basi atarudi kutoka kwenye madhambi yake kama siku aliyozaliwa na mama yake.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Imekuja katika tamko la Muslim:

“Yeyote atakayekuja katika Nyumba hii na asitamke matusi wala kufanya ufuska, basi atarudi kama alivyokuwa siku aliyozaliwa na mama yake.”[1]

Hii Hadiyth ni dalili ya fadhilah za Hajj, ujira wake mkubwa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kwamba mwenye kuhiji anarejea akiwa ametakasika na madhambi yote na safi kabisa kama mtoto mchanga aliyezaliwa hivi sasa, ikiwa atatimiza masharti mawili:

1 – Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… na asitamke maneno ya matusi… ”

Kwa maana ya mambo ya jimaa au yaliyo karibu nayo, kwa maneno au matendo, khaswa akiwa karibu na wanawake, kama vile kushika au kuzungumza kwa lengo la matamanio.

2 – Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”… wala kufanya ufuska… ”

Kwa maana ya kwamba hakutoka ndani ya utiifu wa Allaah kwa kufanya maasi. Miongoni mwa mambo hayo ni yale mambo yaliyokatazwa wakati wa Ihraam. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلَا رَفَثَ وَلَا فُسُوقَ وَلَا جِدَالَ فِي الْحَجِّ

“Atakayekusudia kuhiji, basi asifanye tendo la ndoa na madhambi wala mabishano katika hajj.”[2]

Maana yake ni kwamba yule aliyekusudia Hajj kwa kuingia ndani ya Ihraam, basi ni lazima aheshimu maamrisho ya Allaah, ajiepushe na kila jambo linalopingana na kumtakasia nia Allaah na kuikusudia Nyumba Yake Tukufu. Asizungumze maneno ya matusi, asitende maasi na asibishane kwa ubatili, kwa sababu hayo yanapingana na lengo kuu la Hajj, ambalo ni kumnyenyekea Allaah na kujishughulisha kwa utajo wake na du´aa.

[1] al-Bukhaariy (1449) na Muslim (1350).

[2] 02:197

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 10/05/2025