09. Bishara kwa waislamu kwa kufikiwa na Ramadhaan

Nawausia nyinyi na najiusia nafsi yangu katika mwezi huu uliobarikiwa na katika miezi mingine pia kumcha Allaah. Lakini mwezi huu una sifa maalum Allaah alioubagua nayo, kwani ni msimu wa kheri. Imepokelewa kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimuomba Allaah ajalie kuufikia mwezi wa Ramadhaan. Alikuwa akisema pindi unapoingia mwezi wa Rajab:

”Ee Allaah! Tubarikie Rajab na Sha´baan na utufikishe Ramadhaan.”[1]

Isitoshe imepokelewa kwamba alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwabashiria Maswahabah wake juu ya kuwasili kwake na kuwabainishia fadhilah zake, akisema:

”Enyi watu! Umewakunjieni mwezi mkubwa uliobarikiwa.”

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Imekujieni Ramadhaan – mwezi uliobarikiwa. Allaah (´Azza wa Jall) amewafaradhishieni funga yake. Ndani yake hufunguliwa milango ya mbinguni, hufungwa milango ya Moto na hufungwa mashaytwaan waasi. Ndani yake kuna usiku ulio bora kuliko miezi elfu. Atakayenyimwa kheri yake basi hakika amenyimwa.”[2]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwahimiza Maswahabah wake kufanya juhudi ndani yake kwa matendo mema, ya faradhi na ya kujitolea, swalah na swadaqah, kutoa wema na ihsani, kuwa na subira juu ya utiifu wa Allaah, kuimarisha mchana wake kwa funga na usiku wake kwa kuswali na nyakati zake kwa kusoma Qur-aan na kumtaja Allaah (´Azza wa Jall). Kwa hiyo msiupoteze kwa ghafla na kuupa mgongo, kama ilivyo hali ya watu wa mashaka waliomsahau Allaah ambapo na Yeye akawasahaulisha nafsi zao. Matokeo yake hawanufaiki na kupita kwa misimu ya kheri, hawajui heshima yake na wala hawaithamini thamani yake.

[1] al-Bayhaqiy (07/398) (nr. 3534), al-Bazzaar (01/294), Abu Nu´aym (06/269) na Ibn ´Asaakir (18049). Ni dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf-ul-Jaamiy´” (4395) na ni dhaifu pia kwa mujibu wa mkaguzi wa Shu´biy.

[2] Ahmad (02/230), ´Abdullaah bin Humayd (1429) na an-Nasaa´iy (04/129).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 18
  • Imechapishwa: 28/01/2026