Ndugu wapendwa! Tambueni kuwa swawm ni katika ´ibaadah na utiifu uliobora kabisa. Kumepokelewa mapokezi juu ya fadhilah yake na kumenakiliwa juu yake khabari mbalimbali kati ya watu.

Miongoni mwa fadhilah za swawm ni kwamba Allaah ameiandika juu ya nyumati zote na akaifaradhisha juu yao. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah.”[1]

Lau ingelikuwa sio ´ibaadah tukufu ambayo hakuna viumbe wowote ambao wanajitosheleza nayo kumwabudu Allaah na kutokana na zile thawabu inapelekea juu yake basi Allaah asingeifaradhisha juu ya nyumati zote.

Miongoni mwa fadhilah za kufunga Ramadhaan ni kwamba ni sababu ya kusamehewa madhambi na makosa. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Bi maana kwa kumwamini Allaah na kuridhia faradhi ya swawm juu yake na kutarajia thawabu na ujira. Kwa msemo mwingine si mwenye kuchukia ufaradhi wake na kutilia shaka thawabu na ujira wake. Basi Allaah anamsamehe madhambi yake yaliyotangulia.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah vipindi vitano, ijumaa hadi ijumaa nyingine na Ramadhaan hadi Ramadhaan nyingine ni vyenye kufuta yaliyo baina yake ikiwa mtu atajiepusha na madhambi makubwa.”

Miongoni mwa fadhilah za swawm ni kwamba thawabu zake hazikufungamanishwa na idadi maalum. Bali mfungaji analipwa ujira wake pasi na hesabu. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) amesema: “Matendo yote ya mwanadamu ni yake, isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu mimi na mimi Ndiye nitailipa. Swawm ni kinga. Itapokuwa ni siku ya funga ya mmoja wenu, basi asizungumze maneno machafu wala asipige kelele. Mtu akimtukana au akamgombeza, basi amwambie: “Mimi nimefunga. Mimi nimefunga.” Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake kwamba ile harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski. Mfungaji ana furaha mbili anazofurahi: anapokata swawm anafurahi kwa futari yake na atapokutana na Mola wake atafurahi kwa funga yake.”

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Kila kitendo cha mwanadamu ni chake tendo jema moja linalipwa kwa kumi mfano wake mpaka mara mia saba. “Allaah (Tabaarak wa Ta´la) amesema: “Isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu mimi na mimi Ndiye nitailipa.”

Hadiyth hii tukufu imejulisha juu ya fadhilah za swawm kwa njia nyingi zifuatazo:

1- Allaah ameifanya swawm kuwa ni maalum Kwake kati ya matendo mengine yote. Hayo ni kutokana na utukufu wake mbele Yake na kuipenda na kudhihiri kumtakasia imani Yeye. Kwani swawm ni siri kati ya mja na Mola Wake. Hakuna anayejua isipokuwa Allaah pekee. Mfungaji anakuwa maeneo ambayo hakuna mtu hata mmoja ambapo anaweza kutumia vile Allaah alivyomuharamishia wakati wa funga. Lakini hata hivyo hatumii vitu hivyo kwa sababu anatambua kuwa yuko na Mola ambaye anamuona katika uficho wake. Vitu hivyo vimeharamishwa juu yake na hivyo akaviacha kwa ajili ya Allaah kwa sababu ya kuogopa adhabu Yake na kutamani thawabu Zake. Kwa ajili hiyo ndio maana akawashukuru kwa Ikhlaasw yao hii ambapo akaifanya swawm kuwa ni maalum Kwake kati ya matendo mengine yote. Kwa ajili hii ndio maana akasema:

“Anayaacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu.”

Faida ya sifa hii ya kipekee itaonekana siku ya Qiyaamah. Hayo yamesemwa na Sufyaan bin ´Uyaynah (Rahimahu Allaah):

“Itapokuwa siku ya Qiyaamah basi Allaah atamfanyia hesabu mja Wake na atamlipa zile dhuluma zilizo dhidi yake kati ya matendo mengine yote mpaka pale ambapo hakutobaki kitu isipokuwa tu funga basi Allaah atambebea zile dhuluma zilizobakia juu yake na amwingize Peponi kwa sababu ya swawm.”

[1] 02:183

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 12-15
  • Imechapishwa: 07/04/2020