09. Allaah yuko juu ya mbingu na sisi tuko ardhini

36 – Imesihi kwamba Qataadah amesema:

”Wana wa israaiyl walikuwa wakisema: ”Ee Mola! Wewe uko juu ya mbingu na sisi tuko ardhini. Ni vipi tutajua kuwa umeridhia au umeghadhibika?” Akasema: ”Ninapokuwa radhi nanyi basi Hufanya wale wabora wenu ndio wakakutawaleni na ninapokughadhibikieni basi Hufanya wale waovu wenu ndio wakakutawaleni.”

37 – Imethibiti kwamba Thaabit al-Bunaaniy amesema:

”Daawuud alikuwa akirefusha swalah, kisha akirukuu, kisha akiinua kichwa juu mbinguni kisha akisema: ”Ee Ambaye uko juu ya mbingu. Nimekiinua kichwa Changu kukuelekea, kama ambavo watumwa wanawatazama mabwana wao, Ee Ambaye unaishi juu ya mbingu!”[1]

38 –  Abu Haniyfah amesema:

”Anayepinga kwamba Allaah (Ta´ala) yuko juu ya mbingu amekufuru.”

39 – Maalik amesema:

”Allaah yuko juu ya mbingu na ujuzi Wake uko kila mahali – hakuna kinachojificha Kwake.”[2]

40 – Hammaad bin Zayd amesema kuhusu Jahmiyyah:

”Wanachotaka kusema ni kuwa hakuna mungu yeyote juu ya mbingu.”

41 – Jariyr bin ´Abdil-Hamiyd amesema:

”Maneno ya Jahmiyyah mwanzo wake ni asali na mwisho wake ni sumu. Mambo yalivyo ni kwamba wanachotaka kusema ni kwamba hakuna mungu yeyote juu ya mbingu.”

42 – Bwana mmoja alisema kumwambia Ibn-ul-Mubaarak:

”Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Namukhofu Allaah (´Azza wa Jall) kutokana na wingi nilivyomuomba Allaah dhidi ya Jahmiyyah.” Akasema: ”Usikhofu. Kwani wao wanadai kuwa mungu wako aliye juu ya mbingu si chochote.”

[1] adh-Dhahabiy amesema:

”Cheni ya wapokezi wake ni salama.” (al-´Uluww, uk. 552)

[2] al-Laalakaa’iy (2/401), ´Abdullaah bin Ahmad katika ”as-Sunnah” (1/107) na al-Aajurriy katika ”ash-Shariy´ah”, uk. 289.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 58-60
  • Imechapishwa: 02/06/2024