Muulizaji anataka kujua kile wanachosema wanazuoni waliobobea katika elimu, na si wanazuoni wa upotofu, wale wanaojifanya kuwa ni wanazuoni wala wajinga. Maswali wanatakiwa kuulizwa wanazuoni wenye mwenendo wa kiungu na ambao wamebobea katika elimu. Wao ndio ambao yanazingatiwa maneno na fatwa zao.

Tawiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat ni aina ya tatu miongoni mwa sampuli za Tawhiyd. Nyenginezo mbili ni:

1 – Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Maana yake ni kumpwekesha Allaah kwa matendo Yake, kukiwemo kuumba, kuruzuku, kuhuisha, kufisha na kuendesha ulimwengu.

2 – Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Maana yake ni kumpwekesha Allaah kwa matendo wanayofanya waja ambayo wanayafanya kujikurubisha Kwake, kukiwemo du´aa, swalah, kuchinja na kuweka nadhiri.

3 – Tawiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat. Maana yake ni mtu kumthibitishia Allaah yale majina na sifa alizojithibitishia nazo Mwenyewe. Sambamba na hilo kumtakasa Allaah kutokana na yale mapungufu na kasoro alizojitakasa nazo Mwenyewe. Yote hayo yanatakiwa kufanyika kwa mujibu wa vile ilivyokuja ndani ya Qur-aan na Sunnah. Ukweli wa mambo ni kwamba aina hii inaingai ndani ya Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Kwa ajili hiyo baadhi ya wanazuoni wanaigawanya Tawhiyd katika mafungu mawili peke yake:

1 – Tawhiyd katika utambuzi na uthibitisho. Hii ni Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na Tawiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat. Kwa msemo mwingine inaitwa Tawhiyd ya utambuzi.

2 – Tawhiyd katika matakwa na makusudio. Hii ni Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Hii kwa msemo mwingine huitwa Tawhiyd ya matendo.

Lakini wakati ambapo jambo la kupekua majina na sifa za Allaah lilipokuwa la kawaida katika vizazi vya wale waliokuja nyuma, ndipo wanazuoni wakahitaji kuipambanua sampuli hii na hivyo kuifanya kuwa ni fungu la tatu kwa ajili ya kuwaraddi hawa wapekuzi na kuibainisha haki. Kwa kifupi ni kwamba kwa njia ya jumla Tawhiyd imegawanyika aina mbili:

1 – Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na ndani yake kunaingia Tawiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat.

2 – Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah.

Vigawanyo hivi vinatokana na Qur-aan na Sunnah na sio istilahi zilizozuliwa na watu, kama wanavosema wajinga na watu wenye malengo mabaya.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 24/07/2024