48 – ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinambia: “Sema:

اللَّهُمَّ اهْدِنِي، وَسَدِّدْنِي. وَاذْكُرْ بِالْهُدَى : هِدَايَتَكَ الطَّرِيقَ وَالسَّدَادِ : سَدَادَ السَّهم

“Ee Allaah! Niongoze na unifanye imara”, na pindi unapotaja njia basi kumbuka ile njia ilionyooka, na pindi unapotaja uimara kumbuka uimara unyoofu wa mshale.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Sema:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْهُدَى وَالسَّدَادَ

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba uongofu na uimara.”[1]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Kumuomba Allaah akuongoze maana yake akuongoze na akuwafikishe.

Uimara ni kuwafikishwa katika haki na kuweza kuisibu. Kwa maana nyingine unamuomba Allaah akufanye imara na kuwa na msimamo katika mambo. Imesemekana vilevile ya kwamba huo ni umaalum baada ya ueneaji. Mtu anaweza pia kusema kuwa uongofu unakuwa katika elimu na uimara unakuwa katika matendo.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Na pindi unapotaja njia basi kumbuka ile njia ilionyooka… “

Bi maana yakumbuke hayo mawili wakati wa kuomba kwako du´aa, kwa sababu anayeikusudia njia ilionyooka hapindi kutokana nayo na anayerusha mshale anapupia kulenga shabaha. Vivyo hivyo anayeomba du´aa anapaswa kupupia kuifanya imara elimu yake, kuinyoosha na kushikamana na Sunnah.

[1] Muslim (2725).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 53
  • Imechapishwa: 14/10/2025