05 – kufufuliwa baada ya mauti.

Ahl-us-Sunnah wanaamini msingi wa tano, ambao ni kuamini siku ya Mwisho au kufufuliwa baada ya kufa. Ahl-us-Sunnah wanaamini kuwa majini na watu watakufa na kwamba watafufuliwa. Mtu anaweza kusema ´ufufuo wa Mwisho` na pia mtu anaweza kusema ´siku ya Mwisho`. Yote mawili yametajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah. Siku ya mwisho ni kumetajwa kwa dalili ya Qur-aan na katika baadhi ya Hadiyth kumekuja ufufuo baada kufa.

Ahl-us-Sunnah wanaamini kuwa watu na majini watakufa kisha baada ya hapo watafufuliwa. Halafu waende kulipwa kwa ajili ya matendo yao mema na maovu. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amebainisha hilo pale aliposema:

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa kamwe. Sema: “Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu, bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa kwa yale yote mliyoyatenda; na hayo kwa Allaah ni mepesi.” (64:07)

Ni lazima watu wafufuliwe na kulipwa.

Kwa hivyo siku ya Mwisho ni kule kufufuliwa baada ya kufa. Hapo ndipo watu watalipwa kwa matendo yao, ambaye alitenda mema atalipwa mema na ambaye alitenda maovu atalipwa maovu. Amesema (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى

“Na ni vya Allaah pekee vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ili awalipe [adhabu ya Moto] wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyatenda na ili awalipe wale waliofanya wema kwa [kuwaingiza] Peponi.” (53:31)

Muumbaji ana miadi ambayo ni siku ya Qiyaamah hata kama duniani anaweza kuwaacha. Ikiwa kuna watu watakufa pasi na kuadhibiwa, basi wana miadi. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَلَا تَحْسَبَنَّ اللَّـهَ غَافِلًا عَمَّا يَعْمَلُ الظَّالِمُونَ ۚ إِنَّمَا يُؤَخِّرُهُمْ لِيَوْمٍ تَشْخَصُ فِيهِ الْأَبْصَارُ

“Na wala usidhanie kwamba Allaah ameghafilika na yale wanayoyatenda madhalimu; Hakika anawaakhirisha anawapa muhula kwa ajili ya Siku ambayo macho yatadokoka [kwa kiwewe kubwa].” (14:42)

Bi maana siku ya Qiyaamah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 14
  • Imechapishwa: 16/10/2024