08. Ambaye alikuwa akimwabudu Muhammad, basi hakika Muhammad ameshakufa!

Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ambaye alikuwa akimwabudu Muhammad, basi hakika Muhammad ameshakufa. Na ambaye alikuwa akimwabudu Allaah aliye juu ya mbingu, hakika Allaah yuhai na hafi.”[1]

Ameipokea ad-Daarimiy.

Wakati wa tukio moja ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alikutana na kikongwe ambaye alimsimamisha. Akasimama kuzungumza naye. Bwana mmoja akamwambia: ”Ee kiongozi wa waumini! Umewachelewesha watu kwa ajili ya mwanamke huyu mzee.” Akasema: ”Ole wako! Je, unajua huyu ni nani? Huyu ni mwanamke ambaye Allaah alisikia malalamiko yake kutoka juu ya mbingu saba. Huyu ni Khawlah ambaye Allaah ameteremsha juu yake:

قَدْ سَمِعَ اللَّـهُ قَوْلَ الَّتِي تُجَادِلُكَ فِي زَوْجِهَا وَتَشْتَكِي إِلَى اللَّـهِ

”Hakika Allaah amekwishasikia kauli ya yule mwanamke anayejadiliana nawe kuhusu mumewe na anamshitakia Allaah.”[2]

Ameipokea ad-Daarimiy[3].

´Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Kati ya mbingu ya saba na Kursiy kuna umbali wa miaka mia tano. Kati ya Kursiy na maji kuna umbali wa miaka mia tano. ´Arshi iko juu ya maji, Allaah yuko juu ya ´Arshi hakuna hakuna chochote kinachofichika Kwake miongoni mwa matendo yenu.”[4]

Ameipokea ´Abdullaah bin Ahmad, Ibn Khuzaymah, Ibn-ul-Mundhir, at-Twabaraaniy, al-‘Assaal, at-Twalamankiy, Ibn ´Abdil-Barr, al-Laalakaa’iy na al-Bayhaqiy.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Watu watafufuliwa wakiwa peku, uchi, wakitembea kwa miguu na wakiwa wamesimama kwa muda wa miaka arobaini. Macho yao yakiwa yameelekezwa mbinguni wakingoja hukumu itolewe. Jasho limewafunga kutokana na ukali wa dhiki. Allaah atashuka katika vivuli vya mawingu kutoka ´Arshi hadi kwenye Kursiy.”

Ameipokea na Abu Ahmad al-‘Assaal.

´Abdullaah bin ´Abbaas amesema:

”Fikirini kila kitu, lakini msifikirie kuhusu dhati ya Allaah. Kwani hakika baina ya mbingu hadi kwenye Kursiy Yake kuna nuru elfu saba. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko juu yake.”[5]

Ameipokea Abush-Shaykh katika ”al-´Adhwamah” na al-Bayhaqiy katika ”al-Asmaa’ was-Swifaat”.

Ibraahiym bin al-Hakam bin Abaan amepokea kutoka kwa baba yake, kutoka kwa ´Ikrimah kutoka kwa Ibn ´Abbaas, ambaye amesema kuhusiana na maneno Yake (Ta´ala):

قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ ۖ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ

“Akasema: “Kutokana na ulivyonihukumia kupotoka, nitawakalia katika njia Yako iliyonyooka, kisha nitawaendea mbele yao na nyuma na kuliani kwao na kushotoni kwao na wala hutopata wengi wao ni wenye kushukuru.”[6]

”Hakuweza kusema kutoka juu yao kwa sababu alijua kuwa Allaah yuko juu yao.”[7]

Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Abu Bakr alimwambia ´Umar baada ya kufariki kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Twende kwa Umm Ayman tumtembelee kama vile Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyokuwa akimtembelea.” Walipofika kwake alilia. Wakamuuliza: ”Ni kipi kinacokuliza? Yale yaliyoko kwa Allaah ni bora kwa Mtume Wake.” Akasema: ”Mmesema kweli, lakini ninalia kwa sababu wahy umekatika kutoka juu mbinguni.” Akawafanya nao walie ambapo wakaanza kulia pamoja naye.”[8]

Ameipokea Muslim.

[1] ar-Radd ´alaa Bishr al-Mariysiy, uk. 105. Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa adh-Dhahabiy katika ”al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn”, uk. 56.

[2] 58:1

[3] ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah, uk. 26. adh-Dhahabiy amesema kwamba ”cheni yake ya wapokezi ni salama, hata hivyo yenye kukatika. Abu Yaziyd hakuwahi kukutana na ´Umar.” (al-´Uluww lil-´Aliyy al-Ghaffaar, uk. 113)

[4] Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa dh-Dhahabiy katika “al-´Uluww lil-´Aliyy al-Ghaffaar”, uk. 79, na cheni yake ya wapokezi ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Mukhtaswar-ul-´Uluww”, uk. 103-104.

[5] Abush-Shaykh (1/212) na al-Bayhaqiy katika “al-Asmaa’ was-Swifaat” (2/323).

[6] 07:16-17

[7] Sharh Usuwl I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah (3/396) ya al-Laalakaa’iy.

[8] Muslim (2454).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad bin ´Abdil-Haadiy al-Maqdisiy (afk. 744)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Kalaam ´alaa Mas-alat-il-Istiwaa’ ´alaal-´Arsh, uk. 41-44
  • Imechapishwa: 21/12/2025