Kuna walinganizi wanaolingania katika upotofu. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَجَعَلْنَاهُمْ أَئِمَّةً يَدْعُونَ إِلَى النَّارِ

“Tukawafanya viongozi wanaoita watu Motoni.” (28:41)

أُولَـٰئِكَ يَدْعُونَ إِلَى النَّارِ ۖ وَاللَّـهُ يَدْعُو إِلَى الْجَنَّةِ وَالْمَغْفِرَةِ بِإِذْنِهِ

“Hao wanaita katika Moto, na Allaah anaita katika Pepo na msamaha kwa idhini Yake.” (02:221)

إِنَّمَا يَدْعُو حِزْبَهُ لِيَكُونُوا مِنْ أَصْحَابِ السَّعِيرِ

“Hakika si vyenginevyo anaitia kikosi chake ili wawe watu wa Moto wa uwakao kwa nguvu.” (35:06)

Shaytwaan na wasaidizi wake wanawaita watu kuelekea Motoni. Hawawaambii watu “njooni twende Motoni!”. Badala yake wanawaambia “njooni katika haki na sisi ndio tuko na haki, sisi ndio tuko na elimu na hoja”. Wanawadanganya watu. Mtu ambaye yuko na elimu kidogo na mjinga anadanganyika na mambo haya na anafikiri kuwa ni haki ilihali ni sarabi:

كَسَرَابٍ بِقِيعَةٍ يَحْسَبُهُ الظَّمْآنُ مَاءً حَتَّىٰ إِذَا جَاءَهُ لَمْ يَجِدْهُ شَيْئًا

“… ni kama sarabi jangwani; mwenye kiu hudhania kuwa ni maji, hata anapoyafikia hayakuti kitu chochote.” (24:39)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa fitina itazidi kuwa nyingi na kutakuwepo walinganizi waliosimama kwenye milango ya Motoni. Yule mwenye kuwatii wanamtupa ndani yake. Maswahabah wakasema: “Tueleze sifa zao, ee Mtume wa Allaah.” Akasema:

“Ni watu wenye ngozi kama zetu. Wanazungumza kwa ndimi zetu.”[1]

Huku ndio kutimia kwa fitina ambapo wako kati yetu, kati ya watoto zetu, kati ya miji yetu na wanazungumza lugha moja nasi. Pamoja na yote haya ni watu wanaolingania kwenda Motoni na wanalingania kwenye upotevu. Hili ni jambo limeshuhudiwa na hii leo mnalisikia. Leo mnasikia ulinganizi wa upotevu kwenye vyombo vya khabari na kwenye TV. Humo mtapata ulinganizi wa kwenye upotofu, kuenezwa ´ibaadah za kuabudu makaburi, ukhurafi na wanaeneza kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall). Wanafanya hayo kwa kutumia jina la Tawhiyd. Hawasemi kuwa hii ni shirki. Kinyume chake wanasema kuwa hii ndio Tawhiyd, dini na Sunnah ili wawapake watu mchanga wa machoni:

يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا

”Wanadokezana wenyewe kwa wenyewe maneno ya kupambapamba na ya kudanganya.” (06:112)

[1] Muslim (1847).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Radd Shubuhaat hawl Da´wat-il-Mujaddid, uk. 31-34
  • Imechapishwa: 08/02/2026