07. Mwenye kuweka baina yake na Allaah mkati na kati

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

02 – Mwenye kuweka baina yake na baina ya Allaah wakati na kati akawa anawaomba, kuwataka uombezi na kuwategemea anakufuru kwa maafikiano.

MAELEZO

Anayeweka baina yake na Allaah wakati na kati, kwa mfano akamuomba maiti au aliyemo ndani ya kaburi kama kusema: “Ee fulani! Niombee kwa Allaah.” Pamoja na kwamba aina hii inaingia katika ile aina ya kwanza, lakini hata hivyo ni maalum kuliko hiyo ya kwanza. Shirki ni kumfanyia ´ibaadah asiyekuwa Allaah kwa njia ya jumla. Kama mtu kumuomba mwingine asiyekuwa Allaah, akachinja kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah au akamuwekea nadhiri asiyekuwa Allaah.

Kuhusiana na kichenguzi cha pili hichi ni mtu akaweka baina yake yeye na Allaah wakati na kati kwa madai ya kwamba wanamfikishia mahitaji yake kwa Allaah. Kwa mfano mtu akamwambia aliyemo ndani ya kaburi: “Ee fulani! Niombee kwa Allaah”, “Ee Mtume wa Allaah! Niombee”. Bi maana amemfanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mkati na kati baina yake yeye na Allaah. Hii ni shirki. Kwa sababu amemuomba asiyekuwa Allaah. Mwenye kumuomba asiyekuwa Allaah ameshirikisha. Huyo anakusanywa na maandiko yenye kusema:

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ

“Na wala usiombe badala ya Allaah asiyekunufaisha na wala asiyekudhuru. Na ukifanya [hivyo], basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.”[1]

فَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتَكُونَ مِنَ الْمُعَذَّبِينَ

“Basi usiombe [au kuabudu] pamoja na Allaah mungu mwengine ukaja kuwa miongoni mwa watakaoadhibiwa.”[2]

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

“Hakika shirki ni dhuluma kubwa mno!”[3]

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Na yeyote yule anayeomba [du’aa au kuabudu] pamoja na Allaah mungu mwengine hana ushahidi wa wazi wa hilo; basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake – hakika hawafaulu makafiri.”[4]

Amemuita kuwa ni kafiri.

وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ

“Na siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu.”[5]

وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ

“Na wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende. Mkiwaomba hawasikii maombi yenu na hata wakisikia, basi [wasingeliweza] kukujibuni. Na siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu.”[6]

Allaah ameita yale wayafanyayo kuwa ni shirki.

Kwa hivyo yule mwenye kuweka baina yake na Allaah mkati na kati ambapo akawa anamuomba badala ya Allaah, anamuomba uombezi au anamtegemea anakufuru kwa maafikiano ya waislamu. Hii ni aina ya shirki.

Kutegemea maana yake ni mtu akauegemeza moyo wake kwake na akamwachia mambo yake ili aweze kufikia mahitaji yake.

Kichenguzi cha kwanza kimeenea na hichi cha pili ni maalum zaidi. Kichenguzi cha kwanza ni kushirikisha katika ´ibaadah ya Allaah. Ni mamoja ´ibaadah hiyo iwe ni du´aa, kuchinja, nadhiri, kutii katika uhalalishaji au uharamishaji, Rukuu´ au Sujuud. Kichenguzi cha pili ni maalum. Nacho ni mtu akaweka baina yake yeye na Allaah mkati na kati ambapo akawa anamuomba, kumtaka uombezi na kumtegemea ili kufikia mahitaji yake. Mtu akamfanya maiti kuwa baina yake yeye na Allaah na kusema: “Ee fulani! Niombee kwa Allaah”, “Ee fulani! Nifikishie haja yangu kwa Allaah”. Hili linamuhusu aliye hai vilevile. Kwa mfano akamtegemea kuwa atamuokoa kutokana na Moto, amnusuru na maadui zake, amfanyie wepesi katika riziki, kupata mtoto au kuingia Peponi, mtu huyu amemtegemea katika mambo ambayo hategemewi yeyote isipokuwa Allaah.

Hivyo basi, yule mwenye kuweka baina yake yeye na Allaah mkati na kati, ni mamoja awe hai au maiti, anakuwa mshirikina. Aliye hai anaombwa mambo ambayo anayaweza. Kwa mfano unaweza kumuomba aliye hai akutengenezee gari yako, akukope pesa au kukulimia shamba. Ama kumuomba aliye hai akusamehe dhambi zako, akuokoe na Moto, akukunjulie riziki yako, akunusuru dhidi ya adui yako au asikuzuie kuingia Peponi ni mambo ambayo hayawezi na hayamiliki. Kwa hiyo ni shirki.

Mtu akiweka baina yake na Allaah wakati na kati kwa njia ya kwamba akawa anawaomba badala ya Allaah, anawataka uombezi au anawategemea kwa maana ya kwamba akawaachia mambo yake ili aweze kufikia mahitaji yake, basi anakufuru kwa maafikiano ya waislamu. Ndio maana mtunzi amesema:

“Anakufuru kwa maafikiano.”

Dalili ya hili ni dalili zilezile zenye kusema kuwa kufanya shirki katika ´ibaadah ya Allaah ni kufuru yenye kumtoa mtu katika Uislamu. Dalili ambazo ndani yake mna kuharamisha shirki, kumuomba asiyekuwa Allaah katika mambo yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah ndio dalili zilezile za kichenguzi hichi kinachovunja Uislamu. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ

“Na wala usiombe badala ya Allaah asiyekunufaisha na wala asiyekudhuru. Na ukifanya [hivyo], basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.”[7]

Bi maana usije kuwa katika washirikina.

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Na kwamba maeneo yote ya kuswalia ni [kwa ajili] ya Allaah, basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[8]

قُلْ إِنَّمَا أَدْعُو رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِهِ أَحَدًا

“Sema: “Hakika si vyenginevyo mimi namuomba Mola wangu pekee na wala simshirikishi na yeyote”.”[9]

Kwa hivyo yule mwenye kuweka baina yake yeye na Allaah wakati na kati akawa ni mwenye kuwaomba, kuwataka uombezi au akawategemea kwa njia ya kwamba akawaachia mambo yake ili aweze kufikia mahitaji yake amefanya shirki kwa sababu amemfanyia ´ibaadah asiyekuwa Allaah.

[1] 10:106

[2] 26:213

[3] 31:13

[4] 23:117

[5] 35:14

[6] 35:13-14

[7] 10:106

[8] 72:18

[9] 72:20

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 18-22
  • Imechapishwa: 09/04/2023