07. Maneno mengi yanaufanya moyo kuwa mgumu

52 – Ibn Abiy ´Umar ametukhabarisha: Suyfaan ametukhabarisha:

“Nilimwambia al-Hasan bin ‘Umaarah: “Nilikuwa natamani kumuona Sawwaar bin ´Abdillaah. Nielezee yeye.” Akasema: “Alikuwa hafanyi chochote isipokuwa anamkusudia kwacho Allaah.”

53 – Ibn Numayr ametukhabarisha: Ishaaq bin Sulaymaan ametukhabarisha, kutoka kwa Abu Sinaan, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Ibraahiym, ambaye amesimulia kuwa ´Iysaa bin Maryam (´alayhis-Salaam) amesema:

“Fanyeni uchache wa maneno isipokuwa kwa kumtaja Allaah. Kwani hakika wingi wa maneno huufanya moyo kuwa mgumu.”

54 – al-Huutwiy ametukhabarisha: Wahb bin ´Amr bin ´Abd al-Ahmuusiy ametukhabarisha: Abu Saba’ ´Utbah bin Tamiym ametukhabarisha, kutoka kwa ´Abdullaah bin Abiy Zakariyyaa, ambaye amesema:

“Anayezungumza sana hufanya makosa mengi. Mwenye kufanya makosa mengi kumcha kwake Allaah kunakuwa ni kidogo. Ambaye kumcha kwake Allaah ni kidogo unakufa moyo wake. Ambaye unakufa moyo wake Allaah anamuharamishia Pepo.”

55 – Ibn Numayr ametukhabarisha: ´Ubaydullaah bin Muusa ametukhabarisha: Israa’iyl ametukhabarisha, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Ibraahiym, ambaye amesema:

“Walikuwa wanakaa. Yule aliyenyamaza kwa muda mrefu ndiye anayezingatiwa mbora wao.”

56 – al-Huutwiy ametukhabarisha: al-Waliyd bin Muslim ametukhabarisha, kutoka kwa al-Awzaa´iy, kutoka kwa Yahyaa bin Abiy Kathiyr, ambaye amesema:

“Kamwe usemi wa mtu hausalimiki isipokuwa matokeo yake pia husalimika.”

57 – al-Huutwiy ametukhabarisha: ´Ubayd bin Sulaymaan bin Abiys-Saa-ib ametukhabarisha: Nimemsikia baba yangu akitaja kwamba Ibn Abiy Zakariyyaa amesema:

“Nilijifunza ukimya kwa mwaka mzima.”

58 – al-Huutwiy ametukhabarisha: Baqiyyah ametukhabarisha, kutoka kwa Artwaah bin al-Mundhir, ambaye amesema:

“Mtu alijifunza kunyamaza kutoka kwa watu wenye hekima kwa kokoto; aliviweka mdomoni na havitoi isipokuwa alipokuwa anataka kula au kunywa. Alifanya hivyo kwa miaka arobaini.”

59 – al-Huutwiy ametukhabarisha: al-Waliyd ametukhabarisha, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Yaziyd bin Jaabir, kutoka kwa ´Abdullaah bin Abiy Zakariyyaa, ambaye amesema:

“Kwa miaka kumi na mbili nilikuwa nauchunga ulimi wangu.”

60 – Abu Bakr ametukhabarisha: Abu Khaalid al-Ahmar ametukhabarisha, kutoka kwa Muhammad bin ´Ajlaan, kutoka kwa Muhammad bin Ya´quub, ambaye amesimulia kwamba ´Iysaa bin Maryam (´alayhis-Salaam) amesema:

“Msiongei sana isipokuwa kwa kumtaja Allaah, zisije zikawa ngumu nyoyo zenu. Hakika moyo mgumu uko mbali na Allaah.”[1]

61 – al-Husayn bin Hasan ametukhabarisha: Ibn-ul-Mubaarak ametukhabarisha: Wuhayb, au bwana mwengine, ametukhabarisha, kutoka kwa ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz, ambaye amesema:

“Yeyote anayejumuisha maneno yake kwenye matendo yake huzungumza kidogo.”

[1] Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (1719).

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr Ahmad bin Abiy ´Aaswim ash-Shaybaaniy (a.f.k. 287)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-uz-Zuhd, uk. 15-17
  • Imechapishwa: 25/06/2025