07. Du´aa inayosomwa kabla na baada ya Tasliym

28 – ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Miongoni mwa mambo ya mwisho anayosema baina ya Tashahhud na Tasliym ilikuwa ni:

اللّهُـمَّ اغْـفِرْ لي ما قَدَّمْـتُ وَما أَخَّرْت، وَما أَسْـرَرْتُ وَما أَعْلَـنْت، وَما أَسْـرَفْت، وَما أَنْتَ أَعْـلَمُ بِهِ مِنِّي أَنْتَ المُقَـدِّمُ، وَأَنْتَ المُـؤَخِّـرُ لا إِلهَ إِلاّ أَنْـت

“Ee Allaah! Nisamehe niliyoyatanguliza, niliyoyachelewesha, niliyoyafanya kwa siri, niliyoyafanya kwa dhahiri, niliyochupa mpaka na ambayo Wewe unayajua zaidi kuliko mimi. Wewe ni mwenye kutanguliza na Wewe ni mwenye kuchelewesha – hapana mungu wa haki mwengine isipokuwa Wewe.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Akishatoa salamu, aseme:

اللّهُـمَّ اغْـفِرْ لي ما قَدَّمْـتُ

“Ee Allaah! Nisamehe niliyoyatanguliza… ” [1]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Du´aa hii inasomwa kabla na baada ya salamu kutokana na mapokezi haya mawili. Ni du´aa ya kusamehewa madhambi yaliyotangulia na amuwafikishe kuweza kutubu juu ya yale madhambi yanayokuja huko mbele. Aidha anamuomba Allaah amsamehe yale madhambi aliyoyafanya kwa siri na yale aliyoyafanya hadharani. Inafahamisha kupwekeka kwa Allaah (´Azza wa Jall) Ambaye hakuna mungu mwingine wa haki isipokuwa Yeye na hakuna mwingine anayesamehe madhambi isipokuwa Yeye tu (Subhaanah). Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ

“Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao, basi humdhukuru Allaah wakaomba msamaha kwa madhambi yao. Na nani anayesamehe madhambi isipokuwa Allaah? Na hawaendelei katika waliyoyafanya ilihali wanajua.”[2]

[1] Muslim (771).

[2] 03:135

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 06/10/2025