Abu Hurayrah amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mbali na wale Malaika wanaoandika matendo ya watu Allaah anao Malaika wanaozunguka ardhini wanatafuta vikao vya kumtaja Allaah. Wakipata kikao cha kumtaja Allaah, basi hukaa pamoja nao. Wanapotawanyika, hupanda juu kurudi kwa Mola wao.”[1]

Ameipokea Muslim kutoka kupitia kwa Suhayl bin Abiy Swaalih, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Abu Hurayrah.

Qataadah bin an-Nu´maan ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Wakati Allaah alipomaliza kuwaumba viumbe Wake, alilingana juu ya ´Arshi Yake.”[2]

Ameipokea al-Khallaal kwa cheni ya wapokezi yenye masharti ya al-Bukhaariy na Muslim.

Ibn Mas´uud amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah atawakusanya wa mwanzo na wa mwisho wao katika Siku maalum. Watasimama kwa miaka arobaini huku macho yao yakikodoa juu mbinguni wakisubiri  kuhukumiwe. Allaah atashuka katika kivuli cha mawingu, kutoka kwenye ´Arshi kwenda katika Kursiy.”[3]

Ni Hadiyth nzuri[4]. Abu ´Ubaydah bin ´Abdillaah bin Mas´uud amesimulia kutoka kwa Masruuq, kutoka kwa Ibn Mas´uud.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah alipomaliza kuwaumba viumbe, aliandika Kwake juu ya ´Arshi: ”Hakika rehema Yangu imetangulia ghadhabu Yangu.”[5]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ibn ´Abbaas amesema:

”Abu Dharr alipofikiwa na khabari ya kutumilizwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), alimwambia ndugu yake: ”Niletee khabari ya mtu huyu anayesema eti anafikiwa na wahy kutoka mbinguni.”[6]

Ameipokea al-Bukhaariy.

Abu Waa-il ameeleza ya kwamba Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Bwana mmoja alisema: ”Ee wa Mtume wa Allaah! Ni nini Cheo chenye kusifiwa?” Akasema: “Ni siku ambayo Allaah atashuka juu ya ´Arshi Yake.”[7]

Ameipokea Abu Shaykh katika ”al-´Adhwamah”.

[1] Muslim (2689).

[2] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy kwa mujibu wa Ibn-ul-Qayyim katika “Ijtimaa´-ul-Juyuush al-Islaamiyyah”, uk. 108.

[3] Ibn Khuzaymah (123) na al-Haakim (2/1019-1022).

[4] Nzuri kwa mujibu wa Dhahabiy katika “al-´Uluww” na “kwa uchache ni nzuri, au pengine juu ya hapo zaidi” kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Mukhtaswar-ul-´Uluww”, uk. 110-111.

[5] al-Bukhaariy (3194), Muslim (2751), Ahmad (2/466) na wengineo.

[6] al-Bukhaariy (3861).

[7] Abush-Shaykh (225) na al-Haakim (2/394), ambaye amesahihisha cheni yake ya wapokezi ilihali adh-Dhahabiy ameidhoofisha.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad bin ´Abdil-Haadiy al-Maqdisiy (afk. 744)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Kalaam ´alaa Mas-alat-il-Istiwaa’ ´alaal-´Arsh, uk. 37-39
  • Imechapishwa: 21/12/2025