07. Umoja unatakiwa uwe kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah

Lililo wajibu ni kuwa na umoja juu ya Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhusu yale tunayotofautiana basi tuyarudishe katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakuna mambo ya kusameheana na kubaki juu ya tofauti. Badala yake tuyarudishe katika Qur-aan na Sunnah na kuangalia yale yanayoafikiana na haki tuyachukue, na yenye kuafikiana na kosa tujirudi. Hili ndio la wajibu kwetu. Haitakikani kwa Ummah ukabaki kuwa ni wenye kutofautiana. Huenda wale wanaolingania katika kubaki juu ya tofauti wakataja Hadiyth inayosema:

“Kutofautiana kwa ummah wangu ni rehema.”

Hii ni Hadiyth imepokelewa lakini hata hivyo sio Swahiyh. Tofauti sio rehema. Kinyume chake ni adhabu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ

“Na wala msiwe kama wale waliofarikiana na wakakhitilafiana baada ya kuwajia hoja za wazi.” (03:105)

Tofauti inatawanyisha mioyo na kuufarikanisha ummah. Watu wakishakuwa ni wenye kutofautiana ni jambo lisilowezekana kabisa wakanusuriana na kushirikiana. Kati yao kunakuwa uadui na ushabiki juu ya mapote na makundi yao. Hawawezi wakashirikiana kwa hali yoyote. Hushirikiana pale wanapokuwa na umoja na wote wameshikamana kwa kamba ya Allaah. Hili ndilo alilousia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah ameridhia kwenu mambo matatu; mumwabudu na wala msimshirikishe na chochote, mshikamane nyote kwa kamba ya Allaah na wala msifarikiane na mumnasihi yule ambaye Allaah amemtawalishia jambo lenu.”

Allaah anaridhia kwetu mambo haya matatu. Tunachokilenga katika hayo ni kauli yake:

“… mshikamane nyote kwa kamba ya Allaah na wala msifarikiane…”

Hii haina maana kwamba hakuna tofauti na kufarikiana. Kupatikana kwa tofauti ni maumbile ya mwanaadamu. Maana yake ni kwamba kunapopatikana tofauti au kufarikiana yatatuliwe kwa kurejea katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa kufanya hivo mizozo na tofauti zitaisha. Hii ndio haki.

Kuiacha Qur-aan na Sunnah vikahukumu ni jambo halifupiki tu katika mambo ya mivutano ya kimagomvi ya kimali inayokuwa kati ya watu. Wanasema kuwa kuhukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah ni kuhukumu kati ya watu juu ya mali zao na mivutano yao katika mambo ya kidunia tu. Bali ni kuhukumu baina yao katika kila tofauti na mizozo yote. Mizozo katika ´Aqiydah ni kubaya zaidi kuliko mizozo inayopatikana katika mali. Mizozo katika mambo ya ´ibaadah, halali na haramu ni mibaya zaidi kuliko mizozo inayopatikana katika magomvi ya kimali. Mizozo ya kimali ni sehemu moja wapo miongoni mwa tofauti ambazo ni wajibu kuzitatua kwa Qur-aan. Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) kulikuwa kukitokea tofauti kati yao. Lakini hata hivyo walikuwa ni wepesi kukimbilia kurudi katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hivyo tofauti inaisha. Hata baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufa kulitokea tofauti kati yao kuhusiana na ni nani atayekuwa mtawala baada yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Papohapo walitatua mizozo na kujirudi na kumtawalisha Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) na wakanyenyekea kwake na kumtii. Kwa hivyo tofauti na mfarakano uliokuwa umetokea kuhusiana na ni nani atayekuwa mtawala baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yakawa yameisha. Kama tulivyosema tofauti inatokea kati yao (Radhiya Allaahu ´anhum). Lakini hata hivyo wanarejea katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na baada ya hapo tofauti inaisha.

Kurudi katika Qur-aan kunaondosha chuki na vifundo. Hakuna yeyote mwenye kupingana na Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall). Upande mwingine ukiwaaambia watu njooni katika maoni ya imamu au mwanachuoni fulani hawatokinaika. Lakini ukiwaambia njooni katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – ikiwa kweli wako na imani – watakinaika na watarejea. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Hakika si venginevo kauli ya waumini [wa kweli] wanapoitwa kwa Allaah na Mtume Wake ili awahakumu kati yao; husema: “Tumesikia na tumetii” – na hao ndio wenye kufaulu.” (24:15)

Hivi ndivyo wanavosema waumini. Kuhusu wanafiki haki ikiwa kwao wanakuja hali ya kuwa ni watiifu, na haki ikiwa dhidi yao wanaipa mgongo na kuipuuza kama alivyosema Allaah juu yao. Haifai kwa waumini wakabaki juu ya tofauti walizomo. Inahusiana na tofauti zote; ni mamoja ikiwa ni za mambo ya misingi au ya matawi. Zote hizi zifupumbuliwe kwa Qur-aan na Sunnah.

Ikiwa dalili haikubainika kwa mmoja katika wafanya Ijtihaad wawili na ikawa haijulikani ni maoni yepi yenye nguvu juu ya mengine, katika hali hii hakuna kukemeana kwa yule ambaye atachukua maoni ya imamu fulani. Kwa ajili hiyo ndio maana wanazuoni wamesema:

“Hakuna kukemeana katika mambo ya Ijtihaad.”

Hapa inahusiana na mambo ambayo dalili haikuwa wazi kuonesha iko na nani kwa mmoja katika pande mbili.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 19-21
  • Imechapishwa: 18/05/2021