06. Njia ya mwanafunzi kupita na baadhi ya vitabu anavyotakiwa kuanza navyo

Tumewaona baadhi ya watuwazima wasiokuwa na elimu katika nchi yetu hii wamehifadhi baadhi ya vitabu vya ´Aqiydah kama mfano wa “Usuwl-uth-Thlalaathah”, “Kashf-ush-Shubuhaat”, “Kitaab-ut-Tawhiyd” na “Aadaab-ul-Mashiy ilaas-Swalaah”. Vyote hivi ni katika athari ya Da´wah ya Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) na miongoni mwa baraka zake.

Imaam Su´uud bin ´Abdil-´Aziyz wa mwanzo na Imaam Fayswal bin Turkiy wametoa maamuzi kwamba vitabu hivi visomeshwe katika misikiti yote ya Saudi Arabia. Matokeo yake vikahifadhiwa na watuwazima na wadogo, watu wa kawaida na wanafunzi, kama yanavyotambulika hayo na wengi wanaotilia umuhimu khabari hizi na wazee wengi walioko hivi sasa. Hii ndio siri ya pekee ya nchi hii kubaki safi kutokamana na uchafu wa Bid´ah. Lau watu wa kawaida wasingelikuwa na utambuzi juu ya ´Aqiydah yao, basi wangelikuwa na kitu katika mambo ya Bid´ah na ya shirki. Lakini hata hivyo elimu ni kinga madhubuti. Yule mwenye kujipamba nayo basi anasalimika na shari nyingi.

Ni vigumu kuwekea kikomo njia ambayo mtu anaweza kuifikia elimu kwa njia ya kwamba kila mmoja alazimike kuifuata njia hiyo. Lakini vile tunavoona ni kwamba njia bora ni ile inayofuatwa na wanachuoni wetu (Rahimahumu Allaah). Shaykh na ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Sa´diy (Rahimahu Allaah) amesema juu ya jambo hilo kama ilivyotajwa katika “Fataawaa” zake:

“Kulenga vitabu ambavyo mwanafunzi anatakiwa kujishughulisha navyo kunatofautiana kwa kutofautiana kwa hali na miji. Hali ilio karibu zaidi kutokana na vile tunavyoona sisi ni kwamba mwanafunzi anatakiwa kujitahidi kuhifadhi vitabu vifupivifupi katika kila fani. Akishindwa au hifdhi yake ikawa nyonge juu ya matamshi yake, basi azirudirudi mara nyingi mpaka maana yake ikite moyoni mwake. Kisha aende katika fani nyenginezo zinazoweka wazi na kufasiri zaidi msingi ule aliyoujua. Kama mwanafunzi atahifadhi “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah” ya Shaykh-ul-Islaam [Ibn Taymiyyah], “Thalaathat-ul-Usuwl” na  “Kitaab-ut-Tawhiyd” vya Shaykh Muhammad na inapokuja katika Fiqh akasoma vitabu vifupivifupi vya dalili kama mfano wa “Daliyl-ut-Twalab”, ufupisho wa al-Muqniy´ ya “az-Zaad”, inapokuja katiak somo la Hadiyth “Buluugh-ul-Maram”, katika somo la Nahuw “al-Ajrumiyyah” na akatia bidii kufahamu matini hizi na akarejea vile vitabu vya maelezo au vya fani zake atavyowepesikiwa kuvisoma. Kwa sababu mwanafunzi atapohifadhi misingi basi atakuwa na umiliki mkamilifu wa kuvitambua na vitakuwa wepesi kwake vitabu vya fani vyote, vidogo kwa vikubwa. Yule anayepoteza misingi basi hunyimwa kufika.

Yule ambaye atatilia bidii elimu hii yenye manufaa na akamtaka msaada Allaah, basi Allaah atamsaidia na atambarikia elimu yake. Na yule ambaye wakati wa kutafuta kwake elimu atapita njia isiyokuwa yenye manufaa, basi atajipotezea muda. Hatopata zaidi ya maangamivu. Hayo yanatambulika kwa uzoefu na kwa kuonekana… “

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 29-31
  • Imechapishwa: 04/08/2020