28 – Inatakiwa kuamini kuwa imani ni maneno na matendo, matendo na maneno, nia na lengo.  Inazidi na kupungua. Inazidi vile Allaah anavyotaka na inashuka mpaka hakubaki kitu chochote.

29 – Mbora wa ummah huu baada ya Mitume wake kufa ni Abu Bakr, ´Umar na ´Uthmaan. Namna hii ndivyo ilivyopokelewa kwetu kutoka kwa Ibn ´Umar, ambaye amesema:

“Tulikuwa tukisema na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa kati yetu: “Hakika mtu bora baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Abu Bakr, ´Umar na ´Uthmaan. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiyasikia hayo na wala hayapingi.””[1]

Halafu watu bora baada ya watu hawa ni ´Aliy, Twalhah, az-Zubayr, Sa´d bin Abiy Waqqaas, Sa´iyd bin Zayd, ´Abdur-Rahmaah bin ´Awf na Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah. Wote hawa walikuwa wanastahiki ukhalifah.

Kisha watu bora baada ya hawa ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), karne ya kwanza aliyotumwa kwao – wahajiri wa kwanza na Wanusuraji walioswali katika Qiblah zote mbili.

Halafu watu bora baada ya hawa ni wale waliosuhubiana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku moja, mwezi mmoja, mwaka mmoja au chini au zaidi ya hapo. Watakiwa rehema, zitaje fadhilah zao, jiepushe na kutaja kasoro zao na hatumtaji yeyote katika wao isipokuwa kwa wema. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

 “Wanapotajwa Maswahabah zangu, basi nyamazeni.”[2]

Sufyaan bin ´Uyaynah amesema:

“Mwenye kutamka neno japo moja tu kwa kuwasema vibaya Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi ni mtu anayefuata matamanio.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Maswahabah zangu ni kama nyota; yeyote utakayemfuata, basi utaongozwa.”[3]

[1] al-Bukhaariy (3655).

[2] at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (10/243-244) na Abu Nu´aym (4/108). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Jaamiy´” (545).

[3] Uwongo kwa mujibu wa Ibn Hazm katika “al-Ihkaam fiy Usuwl-il-Ahkaam” (2/251) na iliyozuliwa kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “adh-Dhwa´iyfah” (58).

  • Mhusika: Imaam Abu Muhammad al-Hasan bin Khalaf al-Barbahaariy (kfk. 329)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh-us-Sunnah, uk. 75-77
  • Imechapishwa: 16/12/2024