06. Elimu ya kujua sababu ya kuteremshwa Aayah

Ujuzi wa kutambua sababu ya kuteremshwa Aayah fulani unamsaidia mtu kuweza kuifahamu Aayah. Ujuzi wa sababu unapelekea ujuzi kilichosababishwa na Aayah hiyo. Kwa ajili hiyo maoni sahihi zaidi ya wanazuoni ni kwamba endapo haitambuliki nia ya mwapaji, basi mtu atatazama sababu ya kiapo chake hicho, imechochea nini na nini athari yake. Jengine ni kwamba wanaposema kuwa Aayah fulani imeteremshwa kuhusiana na tukio fulani kunaweza wakati fulani kumaanisha sababu ya kuteremshwa kwake, wakati mwingine kunamaanishwa kwamba tukio hilo linaingia ndani ya Aayah ijapokuwa haikutokea sababu yake.

Wanazuoni wamekhitalifiana juu ya masimulizi ya Swahabah anaposema kwamba Aayah fulani imeteremka kuhusiana na tukio fulani; je masimulizi hayo yanazingatiwa kuwa ni Hadiyth ilioungana, kama kunavyotajwa sababu ambayo Aayah fulani imeteremshwa kwa ajili yake, au yanazingatiwa tu kuwa ni tafsiri? al-Bukhaariy anayazingatia kuwa ni Hadiyth ilioungana na wengine hawafanyi hivo, jambo ambalo ndio uhalisia wa vitabu vingi vya Hadiyth vinavyosimulia Hadiyth zilizounganishwa, ikiwa ni pamoja na “al-Musnad” ya Ahmad. Hata hivyo wote wanayaingiza masimulizi ya Hadiyth zilizounganishwa ikiwa yanataja sababu iliyoteremshwa moja kwa moja baada tu ya Aayah hiyo. Yakishatambulika hayo basi hakuna mgongano wakati mtu anaposema kuwa Aayah fulani imeteremshwa kuhusiana na tukio moja na mwingine akasema kuwa Aayah hiyohiyo imeteremshwa kuhusiana na tukio jingine, muda wa kuwa Aayah hiyo inaweza kuhusiana na yote mawili. Ni kama tafsiri iliyokwishatajwa ya Aayah zenye mifano. Na ikiwa mmoja wapo atasema kuwa Aayah fulani imeteremshwa kwa sababu ya tukio fulani na mwingine akasema Aayah hiyohiyo imeteremshwa kwa sababu ya tukio jingine, masimulizi yote mawili yanaweza kuwa sahihi ikiwa Aayah hiyo imeteremshwa punde tu baada ya matukio yote mawili au kwamba imeteremshwa mara mbili; mara ya kwanza baada ya tukio moja na mara nyingine baada ya tukio jingine.

Aina mbili hizi nilizozitaja kuhusiana na kutofautiana kwa tafsiri na kwamba wakati mwingine zinaweza kutegemea majina na sifa tofauti, wakati mwingine kutegemea na aina mbalimbali ya vile vinavyotajwa na vigawanyo vyake, kama vile mifano. Mara nyingi tafsiri za Salaf ni za aina hii, ingawa mtu anaweza kufikiri kuwa zinagongana.

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 38-41
  • Imechapishwa: 24/03/2025