05. Tofauti kati ya Ahl-us-Sunnah na Murji-ah al-Fuqahaa’ ni ya kihakika au ya kimaana tu?

Swali 5: Je, tofauti kati ya Ahl-us-Sunnah na Murji-ah al-Fuqahaa’ katika matendo ya nyoyo au viungo ni ya kilugha tu au ya kimaana?

Jibu: Baadhi ya watu wamesema kuwa tofauti kati ya Murji-ah al-Fuqahaa’ na Ahl-us-Sunnah ni ya kilugha tu. Mfafanuzi wa ”at-Twahaawiyyah”, ambaye ni Ibn Abiyl-´Izz (Rahimahu Allaah) amesema:

“Tofauti kati ya jopo kubwa la Ahl-us-Sunnah na Abu Haniyfah na maswahiba zake ni ya kilugha tu. Mjadala huu unahusiana na majina na maneno tu usiyopelekea uharibifu katika ´Aqiydah.”

Pia amesema:

“Dalili kuwa tofauti kati yao ni ya kilugha ni kwamba pande zote mbili zinasema kuwa matendo ni wajibu na pande zote mbili zinasema kuwa muislamu akifanya wajibu atapata thawabu na akiacha baadhi ya wajibu au akafanya yaliyoharamishwa, basi ataadhibiwa na kuadhibiwa. Lakini tofauti yao ipo hapa: je, wajibu huu ni sehemu ya imani au hapana? Kikosi kubwa cha Ahl-us-Sunnah wamesema kuwa ni sehemu ya imani, huku Abu Haniyfah na maswahibah zake wakisema kuwa si sehemu ya imani.”

Lakini wakati wa kuzingatia kwa kina mwanafunzi haoni kuwa tofauti hii ni ya kilugha tu katika sura zote. Ni kweli kuwa haipelekei uharibifu wa moja kwa moja katika ´Aqiydah, lakini ina athari zake. Miongoni mwa athari hizo ni zifuatazo:

1 – Kikosi kikubwa cha Ahl-us-Sunnah wameafikiana na Qur-aan na Sunnah kwa maneno na maana na hivyo wakaheshimu dalili za Qur-aan na Sunnah. Lakini  Murji-ah al-Fuqahaa’ wameafikiana na Qur-aan na Sunnah kwa maana lakini wakaenda kinyume kwa maneno. Haifai kwa muislamu kwenda kinyume na dalili za Qur-aan na Sunnah, si kwa maneno wala kwa maana. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ

“Hakika si venginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zaozinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea; ambao wanasimamisha swalah na hutoa sehemu katika yale tuliyowaruzuku.”[1]

Allaah (Ta´ala) amebainisha kuwa matendo haya yote ni sehemu ya imani. Khofu ya moyo anapotajwa Allaah ni matendo ya moyo. Kuongezeka kwa imani kwa kusoma Qur-aan ni matendo ya moyo. Utegemezi kwa Allaah ni matendo ya moyo. Pia kuna matendo ya viungo kama kufanya sababu na kutoa mali kwa ajili ya Allaah. Yote haya yameitwa kuwa ni imani. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ

”Hakika hapana vyengine waumini ni wale waliomwamini Allaah na Mtume Wake kisha wakawa si wenye shaka na wanapambana Jihaad kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Allaah. Hao ndio wakweli.”[2]

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana kati yao kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kwa kujisalimisha.”[3]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imani ni tanzu sabini na kitu.”

Upokezi wa al-Bukhaariy unasema:

“Imani ni tanzu sitini na kitu. Ya juu yake kabisa ni neno “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” na ya chini yake ni kuondosha chenye kuudhi njiani. Hayaa ni tanzu pia ya imani.”[4]

Hadiyth hii ni katika dalili zenye nguvu dhidi ya Murji-ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameigawa imani katika sehemu zaidi ya sabini ambapo akatoa mfano wa maneno ya ulimi kuwa ni tamko la Tawhiyd, akatoa mfano wa matendo ya viungo kuwa ni kuondoa chenye kuudhi njiani, akatoa mfano wa matendo ya moyo kuwa ni hayaa. Hayaa ni sifa ya ndani inayomsukuma mtu kufanya mema na kujiepusha na maovu.

Tanzu ya juu kabisa ya imani ni neno la Tawhiyd na tanzu ya chini kabisa ni kuondosha chenye kuudhi njiani. Tanzu za imani zinapishana kwa kiwango. Kuna zile zilizo karibu na shahaadah na zile zilizo karibu na kuondoa chenye kuudhi njiani. Swalah ni tanzu, hajj ni tanzu, zakaah ni tanzu, swawm ni tanzu, kuwafanyia wema wazazi ni tanzu, kuunga undugu ni tanzu, jihaad katika njia ya Allaah ni tanzu, kuamrisha mema ni tanzu, kukataza maovu ni tanzu, kufanya ihsani kwa jirani ni tanzu na tanzu nyenginezo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameviingiza vyote hivi katika maana ya imani. Basi vipi mtu aseme kuwa matendo hayahusiani na imani?

Aidha miongoni mwa dalili zenye nguvu kuwa matendo ni sehemu ya imani ni Hadiyth ya wajumbe wa ´Abdul-Qays aliyopokea al-Bukhaariy na Muslim:

“Wajumbe wa ´Abdul-Qays walifika kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Sisi tunatoka mbali na baina yetu na wewe kuna makafiri Mudhwar. Hivyo hatuwezi kufika kwako isipokuwa katika miezi mitakatifu. Tuamrishe jambo ambalo tutalifanya na kuwaeleza walio nyuma yetu.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ninakuamrisheni mambo manne na ninawakatazeni mambo manne: Ninakuamrisheni kumuamini Allaah pekee. Mnajua nini maana ya kumuamini Allaah pekee? Ni kushuhudia kwamba hapana munug wa haki isipokuwa Allaah pekee, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kutoa khmusi ya ngawira mnayopata.”

Kwa hivyo akaamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) imani kwa matendo ya viungo vya mwili, kitu ambacho ni dalili ya wazi kuwa imani inajumuisha matendo ya viungo vya mwili.

Kwa hivyo kikosi kikubwa cha Ahl-us-Sunnah wamefanya adabu na dalili za Qur-aan na Sunnah na wakaingiza matendo katika maana ya imani, ilihali Murji-ah al-Fuqahaa’ wameenda sambamba na maandiko kimaana lakini wakaenda kinyume nayo kwa maneno. Haifai kwa mtu kwenda kinyume na dalili za Qur-aan na Sunnah, si kimaneno wala kimaana. Bali ni wajibu wake kuyafuata matini zote kwa maneno na maana.

2 – Tofauti ya Murji-ah al-Fuqahaa’ na kikosi kikubwa cha Ahl-us-Sunnah ilifungua mlango kwa Murji-ah waliochupa mipaka. Murji-ah al-Fuqahaa’ waliposema kuwa matendo si sehemu ya imani, ingawa ni wajibu, walifungua mlango kwa Murji-ah waliochupa mipaka ambao walikuwa wakisema matendo si wajibu wala hayatakikani. Kwa hiyo Murji-ah waliochupa mipaka wamesema kuwa swalah, swawm, zakaah na hajj yoye si wajibu, kwamba ambaye amemjua Mola wake kwa moyo wake ni muumini mwenye imani kamili na ataingia Peponi pale mwanzoni kabisa na kwamba matendo si muhimu. Ambao amewafungulia mlango ni Murji-ah al-Fuqahaa’.

3 – Tofauti ya Murji-ah al-Fuqahaa’ na kikosi kikubwa cha Ahl-us-Sunnah wamewafungua mlango watenda madhambi mazito na waasi na wakajiunga nao. Murji-ah al-Fuqahaa’ waliposema kuwa imani ni kitu kimoja kisichoongezeka wala kupungua, kwamba imani ya watu wa ulimwenguni kote na waja wa mbinguni ni moja, wakajitokeza watenda madhambi mazito. Mfano fasiki, mlevi na mchawi anakuja na kusema: “Mimi ni muislamu na nina imani kamili. Imani yangu ni kama ya Jibriyl, Mikaaiyl, Abu Bakr na ´Umar”. Wanaporaddiwa kwamba ni vipi wanaweza kusema kuwa wana imani kama ya Abu Bakr na ´Umar ambao wana matendo makubwa, wanajibu kwa kusema kwamba matendo hayana mahusiano wowote na imani na kwamba wanasadikisha kama ambavo Abu Bakr na Jibriyl wanavosadikisha, jambo ambalo ni batili kubwa kabisa. Kwa ajili hiyo Hadiyth inasema:

“Lau ingelipimwa imani ya Abu Bakr na imani ya watu wa ardhini basi ingelikuwa nzito zaidi.”

Maana yake  ni kwamba wakiondolewa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Ni vipi basi mtu anaweza kusema kuwa imani ni kitu kimoja na kwamba imani ya viumbe wa mbinguni na viumbe wa ardhini ni moja?

4 – Masuala ya kufanya uvuaji katika imani. Mtu kusema ”Mimi ni muumini – Allaah akitaka”. Murji-ah al-Fuqahaa’ wanakataza mtu kufanya hivo kwa sababu wanaona kuwa imani kitu kimoja; kusadikisha. Wanasema kuwa wewe unajijua kuwa ni mwenye kusadikisha ndani ya moyo. Kwa nini basi useme kuwa ni muumini – Allaah akitaka. Kwa mujibu wao wanaona kuwa mwenye kusema hivo ni mwenye kutilia shaka imani yake. Kwa hiyo wanawaita waumini ambao wanafanya uvuaji katika imani yao ”wenye mashaka”.

Kwa hiyo wewe unajua ndani ya nafsi yako kuwa wewe ni mwenye kusadikisha, kama vile unavyojua kuwa umesoma al-Faatihah, kama unavyojua kuwa unampenda Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na kuwachukia mayahudi. Basi vipi unasema: “Mimi ni muumini – Allaah atataka”? Bali unatakiwa kusema: “Mimi ni muumini.” Thibitisha na usiwe na shaka katika imani yako. Upande wa pili kikosi kikubwa cha Ahl-us-Sunnah wanatoa ufafanuzi na kusema: Ikiwa mtu atasema: “Mimi ni muumini – Allaah atataka” akikusudia kuwa ana shaka katika msingi wa imani yake, basi hili ni jambo lisilokubalika, kwa sababu msingi wa imani ni kusadikisha kwa moyo. Lakini ikiwa mtu atazingatia matendo, mambo ya wajibu ambayo Allaah amefaradhisha na makatazo ambayo Allaah amekataza na akatambua kuwa matawi ya imani ni mengi na majukumu ni makubwa, basi hawezi kujisifu kuwa amekamilisha yote. Badala yake anatakiwa ajihesabu kuwa na mapungufu na ajione kuwa hajatimiza kikamilifu. Kwa hiyo akisema: “Mimi ni muumini – Allaah atataka” basi shaka yake inahusiana na matendo yake na hivyo halina tatizo. Bali ni jambo zuri kufanya hivo. Vilevile ikiwa mtu anakusudia kuwa hajui mwisho wake utakuwa vipi, kwani mwisho wa mtu anaujua Allaah pekee, basi hapana vibaya kufanya uvuaji katika imani. Kadhalika hapana vibaya ikiwa mtu anataka kupata baraka kwa kutaja jina la Allaah.

Kwa hivyo hizi ni miongoni mwa athari za tofauti kati yao, na ingawa hazileti uharibifu katika ´Aqiydah, zinathibitisha kuwa tofauti si ya kilugha tu.

[1] 08:02-04

[2] 49:15

[3] 04:05

[4]al-Bukhaariy (9) na Muslim (35).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah wa Ajwibah fiy-Iymaan wal-Kufr, uk. 14-20
  • Imechapishwa: 01/01/2026