05. Mwache Allaah pekee ndiye ajue ´ibaadah yako Kwake

20 – Abu Bakr bin Abiyn-Nadhwr amenihadithia: Mu’ammil ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan, ambaye ameeleza:

“Alikuwa mtu mmoja miongoni mwa Wanusuraji akisema: ”Ee Allaah! Nipe ukumbusho uliositirika mimi na wana wangu na usitupunguzie chochote kwa hilo mbele Yako.”

21 – at-Twayyib bin Ismaa´iyl amenihadithia kwamba al-Khaliyl bin Ahmad alikuwa akiomba du´aa kwa kusema:

“Ee Allaah! Nifanye kuwa mbele Yako miongoni mwa viumbe Wako wa juu zaidi, nifanye katika nafsi yangu kuwa miongoni mwa viumbe Wako wa chini kabisa na nifanye mbele ya watu kuwa miongoni mwa viumbe Wako wa wastani.”

22 – Ahmad bin Ibraahiym na wengine wametuhadithia, kutoka kwa Khalaf bin Tamiym: Nimemsikia Sufyaan ath-Thawriy akisema:

“Nililiona moyo wangu ukitengemaa huko Makkah na Madiynah pamoja na watu wageni – watu wa masikini na wenye taabu.”

23 – Salamah bin Shabiyb al-Kilaabiy ametuhadithia, kutoka kwa ´Amr bin ´Aaswim al-Kilaabiy: Ja´far bin Sulaymaan ametuhadithia:

“Sipendi yeyote anitambue kwa utiifu wangu kwake isipokuwa Yeye tu.”

24 – Ahmad bin Ibraahiym ametuhadithia: Salamah bin ´Iqaar au mtu mwingine amenihadithia:

”Wakati Ibn-ul-Mubaarak alipofika mji wa al-Miswiswah aliulizia kuhusu Muhammad bin Yuusuf al-Aswbahaaniy ambapo akamwambia: “Miongoni mwa fadhilah zako ni kwamba hutambuliki.”

25 – Ibraahiym bin Sa´iyd ametuhadithia: Abu Tawbah ametuhadithia: ´Atwaa’ bin Muslim ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, ambaye amesema:

”Hakika nimemuona kwa Ibraahiym jambo ambalo sidhani kama nitaliona kwa mtu mwengine.” Akasema: ”Ni nini?” Nikasema: ”Nilimwona akiwa ameketi na wageni. Halafu nikamwendea Ibraahiym na kumuuliza juu ya hilo, ambapo akasema: “Nilikuwa nimeketi karibu nao, nikachukia watu waone kuwa naondoka hapo kwa sababu najiona kuwa mimi ni mbora kuliko wao. Kwa ajili hiyo nikaketi nao.”

26 – Abu Ja´far al-Aadamiy ametuhadithia: Muhammad bin Kathiyr ametuhadithia, kutoka kwa Sahl bin Shu´ayb, kutoka kwa ´Abdul-A´laa, kutoka kwa Nawf, ambaye ameeleza kuwa amemsikia ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) akisema:

“Twubaa kwa wale wanaoyapa nyongo maisha ya dunia na wakajipinda kuitafuta Aakhirah! Hao ni watu waliouchukua ardhi kuwa ni zulia, mavumbi yake kuwa ni godoro, maji yake kuwa ni manukato, Kitabu kuwa ni nembo yao na du´aa kuwa ni mavazi yao ya ndani. Wamemkopesha Allaah mkopo kwa kufuata mwenendo wa al-Masiyh ´Iysaa bin Maryam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

27 – Kutokea hapo Yahyaa bin Sulaym ametuhadithia: Nimemsikia Shibl bin ´Abbaad: Nimemsikia Abut-Twufayl: Nimemsikia ´Aliy bin Abiy Twaalib akisema:

“Imeikujieni fitina ya giza, kipofu na iliyotulia – hawatosalimika nayo isipokuwa mwenye usingizi.” Akaulizwa: “Ee Abul-Hasan, ni kina nani hao mwenye usingizi?” Akasema: “Ni yule ambaye watu hawajui nini kilicho moyoni mwake.”

28 – Muhammad bin al-Husayn ametuhadithia: Ahmad bin Sahl al-Urduniy ametuhadithia: Silm, ambaye alikuwa mtu muheshimiwa, amenihadithia: Ibraahiym bin Adham amenambia:

“Sikuwahi kushinda katika ulimwengu kamwe isipokuwa mara moja. Nililala usiku katika moja ya misikiti ya vijiji vya Shaam; na ilikuwa kwenye tumbo la mto. Muadhini akakokota miguu yangu mpaka akanitoa nje ya msikiti.”

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa (afk. 281)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Khumuul wat-Tawaadhwu´, uk. 46-54
  • Imechapishwa: 22/01/2026