35 – Ibn Abiy ´Umar ametukhabarisha: Sufyaan ametukhabarisha, kutoka kwa Ibn Abiy Khaalid, kutoka kwa ´Abdul-Malik bin ´Umayr, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin ´Abdillaah bin Mas´uud, ambaye ameeleza kuwa ´Abdullaah bin Mas´uud alimuusia mwanae ´Abdur-Rahmaan yafuatayo:

“Mwanangu mpendwa! Ninakuamrisha kumcha Allaah, linda ulimi wako, lia juu ya dhambi yako na ikutoshe nyumba yako.”

36 – Shaykh mmoja Makkah ametukhabarisha: Ibn Abiy Uways ametukhabarisha, kutoka kwa Ibn Wahb, kutoka kwa Maalik – yaani Ibn Anas – kutoka kwa Sa´iyd bin Abiy Hind, ambaye amesema:

“Naona kuwa kunyamaza ni kugumu zaidi kuliko kuongea.”

37 – Husayn ametukhabarisha: Ibn-ul-Mubaarak ametukhabarisha, kutoka kwa Ma´mar, kutoka kwa Hammaam bin Munabbih, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

“Neno zuri ni swadaqah.”[1]

38 – Abu Muusa ametukhabarisha: ´Abdur-Rahmaan ametukhabarisha: Israa’iyl ametukhabarisha, kutoka kwa Sa´iyd bin Masruuq, kutoka kwa Mundhir ath-Thawriy, kutoka kwa ar-Rabiy´ bin Khuthaym, ambaye amesema:

“Jihadhari na ulimi wako, ee Bakr bin Maa’iz, isipokuwa kwa yaliyo na manufaa kwako na si dhidi yako. Hakika mimi ninawatuhumu watu katika dini yangu.”

39 – Abu Bakr ametukhabarisha: Abu Usaamah ametukhabarisha: Sufyaan ametukhabarisha, kutoka kwa Abul-Muhajjal, kutoka kwa Ibn ´Imraan bin Hittwaan, kutoka kwa baba yake, ambaye ameeleza kwamba Abu Dharr amesema:

“Kunyamaza ni bora kuliko kuzungumza mabaya.”

40 – Husayn bin Hasan ametukhabarisha: Ibn-ul-Mubaarak ametukhabarisha, kutoka kwa Abul-Ashhab, kutoka kwa al-Hasan, aliyesema:

“Walikuwa wakisema kuwa ulimi wa mwenye hekima uko nyuma ya moyo wake; anapotaka kusema jambo, basi anarejea kwenye moyo wake. Ikiwa ni kwa manufaa yake, basi anayasema, na ikiwa ni dhidi yake, anayazuia. Moyo wa mjinga uko kwenye ncha ya ulimi wake. Harejei kwenye moyo wake. Kinachokuja kwenye ulimi wake ndicho anachozungumza.”

Abul-Ashhab amesema:

“Asiyechunga ulimi wake hakuielewa dini yake.”

41 – Abu Muusa ametukhabarisha: ´Abdur-Rahmaan ametukhabarisha: Sulaymaan bin al-Mughiyrah ametukhabarisha, kutoka kwa Humayd bin Hilaal, ambaye ameeleza kuwa ´Abdullaah bin ´Amr amesema:

“Achana na kile kisichokuhusu na usiongelee kile kisichokuhusu. Ulinde ulimi wako kama unavyoilinda fedha yako.”

42 – Husayn bin Hasan ametukhabarisha: Ibn-ul-Mubaarak ametukhabarisha: Rabaah bin Zayd ametukhabarisha: ´Abdullaah bin Sa´iyd bin Abiy ´Aaswim ametukhabarisha: Nimemsikia bin Munabbih akisema:

“Uislamu bora ni kukaa kimya, ili watu wasalimike nawe.”

43 – Husayn bin Hasan ametukhabarisha: Ibn-ul-Mubaarak ametukhabarisha: Ibn ´Ayyaash ametukhabarisha: ´Aqiyl bin Mudrik ametukhabarisha, kutoka kwa Abu Sa´iyd, ambaye ameeleza:

“Bwana mmoja alimwendea na kusema: ”Niusie.” Akasema: “Nakuusia kumcha Allaah na lazimiana na ukimya. Hivyo ndivyo utamshinda shaytwaan.”

[1] al-Bukhaariy (2707) na Muslim (1009).

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr Ahmad bin Abiy ´Aaswim ash-Shaybaaniy (a.f.k. 287)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-uz-Zuhd, uk. 12-13
  • Imechapishwa: 25/06/2025