05. Hadiyth ”Wanapishana kwenu Malaika wa usiku na Malaika wa mchana… “

Hadiyth ya tatu

إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ

“Kwake Yeye linapanda neno zuri na kitendo chema hukiinua juu.”[1]

19 – Ahmad bin Hibatillaah ametukhabarisha, kutoka kwa ´Abdul-Mu´izz bin Muhammad al-Harawiy: Tamiym bin Abiy Sa´iyd al-Jurjaaniy ametuhadithia: Muhammad bin ´Abdir-Rahmaan al-Kanjaruudhiy ametuhadithia: Abu ´Amr bin Hamdaan ametuhadithia: Abu Ya´laa al-Mawsiliy ametuhadithia: Daawuud bin ´Amr ametuhadithia: Ibn Abiyz-Zinaad ametuhadithia, kutoka kwa al-A´raj, kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

 “Wanapishana kwenu Malaika wa usiku na Malaika wa mchana. Wanakusanyika katika swalah ya Fajr na swalah ya ´Aswr. Halafu hupanda wale waliolala kwenu ambapo Mola wenu Anawauliza – ilihali ni mjuzi zaidi kuliko wao: “Mmewaachaje waja Wangu?” Wanasema: “Tumewaacha na huku wanaswali na tumewaendea na huku wanaswali.”[2]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

20 – Allaah (Ta´ala) amesema:

تَعْرُجُ الْمَلائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ

“Malaika na Roho [Jibrily] wanapanda Kwake katika siku kiasi chake ni miaka elfu khamsini.”[3]

Kitenzi (يَصْعَدُ) na (تَعْرُجُ) vina maana moja, nayo ni kupanda. Kunaingia vilevile ile safari ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupanda juu kwa Mola wake, Malaika wa mauti kupanda juu kwa Mola wake baada ya kumpiga Muusa (´alayhis-Salaam) ambapo likatoka jicho lake na roho kupanda juu ya mbingu ambapo yuko Allaah (Ta´ala).

21 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mja yeyote muumini anayetoa swadaqah kutoka katika pato zuri – na wala hakuna kinachopanda kwa Allaah isipokuwa kilicho kizuri – isipokuwa Allaah anaiweka kwenye mkono Wake wa kuume na anailea kama anavyolea mmoja wenu kitekli chake ambapo tende inakuwa kama mlima mkubwa.”[4]

22 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu Mola wake:

”Mimi Nimejitosheleza kutokana na mshirika. Hakuna chochote katika kujionyesha kinachopanda Kwangu.”

Yote haya ni mapokezi Swahiyh.

 23 – Maalik bin Diynaar amesema:

”Nimesoma katika baadhi ya vitabu vilivyoteremshwa kuwa Allaah anasema: ”Ee mwanadamu! Kheri Zangu zinakushukia na shari zako hupanda Kwangu. Wala Malaika mtukufu haachi kupanda Kwangu kutoka kwako akiwa na matendo yako maovu.”

Zipo Hadiyth na mapokezi mengi juu ya maudhui haya.

[1] 35:10

[2] al-Bukhaariy (7429).

[3] 70:4

[4] al-Bukhaariy (7430).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 46-49
  • Imechapishwa: 29/05/2024