Swali 4: Murji-ah wamegawanyika aina ngapi? Tunaomba ututajie I´tiqaad zao katika suala la imani.

Jibu: Murji-ah wamegawanyika aina mbili:

1 –  Waliovuka mipaka, nao ni Jahmiyyah na kiongozi wao ni Jahm bin Swafwaan ambaye alieneza madhehebu nne za kizushi:

1 – ´Aqiydah ya kukanusha sifa, ambayo ilichukuliwa na wafuasi wake Jahmiyyah.

2 – ´Aqiydah ya Irjaa´, ambayo ilichukuliwa na Murji-ah.

3 – ´Aqiydah ya Jabr, kwamba mja ametenzwa nguvu kwa matendo yake, ambayo ilichukuliwa na Jabriyyah.

4 – ´Aqiydah ya kwamba Pepo na Moto vitateketea.

Hizi ni imani nne ambazo Jahm alizieneza.

Murji-ah waliochupa mipaka ´Aqiydah yao inapokuja katika imani ni utambuzi peke yake. Maana yake ni kwamba inatosha kumtambua Mola ndani ya moyo. Kwa maana nyingine ikiwa mtu atamjua Mola kwa moyo wake ni muumini na hakufuru isipokuwa ikiwa atamkanusha Mola wake kwa moyo wake. Kwa mujibu wa ´Aqiydah hiyo wanazuoni wakawalazimisha kwamba Ibliys ni muumini, kwa sababu anamtambua Mola wake. Allaah (Ta´ala) amesema ya kwamba Ibliys alisema:

قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ

”Akasema: ”Mola wangu! Basi Nipe muhula mpaka siku watakayofufuliwa.”[1]

Fir´awn pia atakuwa ni muumini kwa sababu anamjua Mola wake kwa moyo wake. Allaah (Ta´ala) amesema juu yake na wafuasi wake:

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا ۚ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ

“Wakazikanusha na hali kuwa nafsi zao zimeziyakinisha kwa dhulma na majivuno; basi tazama vipi ilikuwa hatima ya mafisadi.”[2]

Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika ”al-Kaafiyah ash-Shaafiyah” ametaja sura ndefu kuhusu kueleza imani ya Murji-ah waliochupa mipaka na akasema:

”Alificha hili kwa muda kisha alilikiri na akaonyesha kwamba ´Aqiydah yao ni kumtambua Mola kwa moyo tu na kwamba mtu akifanya vitendo vya ukafiri bado hakiathiri kitu imani yake.”

Ina manaa kwamba mtu akimtukana Allaah, kumtukana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuitukana dini ya Uislamu, kuwaua Mitume, waja wema, akabomoa misikiti na akafanya maovu yote, hatakuwa kafiri muda wa kuwa anamjua Mola wake kwa moyo wake. Hii ndio ´Aqiydah mbovu kabisa ilyotajwa katika kuitambulisha imani. Pia ndio ´Aqiydah ya Abul-Husayn as-Swaalihiy katika Qadariyyah.

´Aqiydah inayofuata kwa uovu ni ile ya Karraamiyyah wanaosema kwamba imani ni kusema kwa ulimi pekee. Kwa maana nyingine ni kwamba anayetamka shahaadah kwa ulimi wake, basi anakuwa muumini hata kama ni mwenye kupinga kwa moyo wake na isitoshe wanamzingatia kuwa ni muumini mwenye imani kamili. Wanaona kuwa ikiwa ni mwenye kukadhibisha kwa moyo wake, huyo ni mwenye kuwekwa Motoni milele. Kwa mujibu wa ´Aqiydah yao ni kwamba muumini mwenye imani kamili atadumu Motoni milele, ´Aqiydah ambayo ni mbaya kabisa inayofuata baada ya ile ya Jahm katika ubaya.

Murji-ah al-Fuqahaa´ ambao ni watu wa Kuufah kama vile Abu Haniyfah (Rahimahu Allaah) na wafuasi wake. Mtu wa kwanza aliyesema kuwa imani haingii katika imani ni Hammaad bin Abiy Sulaymaan ambaye ni mwalimu wa Imaam Abu Haniyfah. Abu Haniyfah ana riwaya mbili katika kuitambulisha imani.

1 – Kusadikisha kwa moyo na kusema kwa ulimi, nayo ndio inayofanyiwa kazi na wafuasi wake wengi.

2 – Kusadikisha kwa moyo tu. Kuhusu kutamka kwa ulimi ni nguzo ya ziada iliyo nje ya utambulisho wa imani.

Kwa mujibu wa riwaya ya pili anaenda sambamba na ´Aqiydah ya Maaturiydiyyah wenye kuona kuwa imani ni kusadikisha kwa moyo tu. Hata hivyo wanaona kuwa matendo kama swalah, zakaah, swawm na hijjah yanahitajika. Wanaona kwamba wajibu ni wajibu na haramu ni haramu. Anayefanya wajibu anastahiki kulipwa thawabu na sifa nzuri. Anayefanya madhambi makubwa anastahiki adhabu na kutekelezewa adhabu ya kidini. Lakini hawaoni kama matendo ni sehemu ya imani. Wanasema kuwa mtu ana majukumu mawili: jukumu la imani na jukumu la matendo na kimoja katika viwili hivyo hakihusiani na utambulisho wa kingine.

Ahl-us-Sunnah wengi wanaona kuwa matendo ni katika imani na ni sehemu yake. Matendo ni wajibu na ni sehemu ya imani. Lakini Murji-ah al-Fuqahaa´ wanasema kuwa matendo ni wajibu lakini si sehemu ya imani. Kwa ajili hiyo wako waliosema kuwa tofauti makinzano kati yao na kikosi kikubwa cha Ahl-us-Sunnah ni ya kimatamshi tu. Hayo yamesemwa na mfafanuzi wa ”at-Twahaawiyyah”. Sahihi ni kwamba sio tofauti ya kimatamshi tu.

[1] 38:79

[2] 27:14

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah wa Ajwibah fiy-Iymaan wal-Kufr, uk. 10-13
  • Imechapishwa: 01/01/2026