Kisha baada ya Aayah hii akasema (Subhaanah):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعاً الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لا إِلَهَ إِلاَّ هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ فَآمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الْأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ

“Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote wa [Yule] ambaye pekee anao ufalme wa mbingu na ardhi! Hapana mungu wa haki ila Yeye – Anahuisha na anafisha. Basi mwaminini Allaah na Mtume Wake, ambaye hajui kuandika wala kusoma, ambaye anamwamini Allaah na maneno Yake na mfuateni ili mpate kuongoka.”[1]

Ameweka wazi (Subhaanah) kupitia Aayah hii kwamba amemtuma Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa watu wote wakiwemo waarabu, wasiokuwa waarabu, waume, wake, majini, watu, matajiri, mafukara, watawala na raia. Amebainisha (Subhaanah) kwamba hakuna uongofu isipokuwa kwa yule mwenye kumwamini na akamfuata. Kwa hivyo hayo yakafahamisha kuwa makundi yote yasiyomwamini na yasiyomfuata ni makafiri na wapotofu. Imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa amesema:

“Nabii alikuwa akitumwa kwa watu wake pekee na mimi nimetumwa kwa watu wote.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Naapa kwa Ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake. Hatosikia yeyote kuhusu mimi si myahudi wala mnaswara kisha akafa na asiamini yale niliyotumilizwa nayo isipokuwa atakuwa ni katika watu wa Motoni.”

 Zipo Aayah na Hadiyth nyingi zenye maana kama hii.

Itambulike kuwa ile haki iliokuweko katika Shari´ah ya Tawraat na Injiyl iko pia katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au ambayo ni bora na kamilifu zaidi. Amesema (´Azza wa Jall):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.”[2]

[1] 07:158

[2] 05:03

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/articles/78/الاسلام-هو-دين-الله-ليس-له-دين-سواه
  • Imechapishwa: 06/10/2021