04. Kuwa na subira na taraji malipo kwa Allaah

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaweza kuwa wachache katika nyakati fulani kama ambavyo vilevile wanaweza kuwa wengi na pengine wasiwepo isipokuwa idadi ya watu wachache tu. Lakini ndani yao mna baraka na kheri. Kwa kuwa wao ndio wamo katika haki. Waliyo juu ya haki hawaogopi uchache na wala hachelei kwa kuwepo wingi wa maadui. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ ۚ وَحَسُنَ أُولَـٰئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume, basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha ambao ni Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje hao kuwa ni rafiki zake!”[1]

Amuogope nani yule ambaye marafiki zake watakuwa ni watu hawa ambao Allaah amewaneemesha ambao ni Manabii, wakweli, mashahidi na waja wema? Kinachotakiwa ni kuwa na subira kwa kutarajia kupata radhi za Allaah. Lakini hata hivyo jambo hili linahitaji kwa mja awe na ujuzi na elimu juu ya njia ya watu hawa. Halafu awe na subira juu yake na astahamili maudhi ya wale wanaoenda kinyume naye.

Ambaye atakuwa ni mwenye kusubiri katika njia ya Allaah, dini ya haki na Sunnah atapata maudhiko na lawama mbalimbali kutoka kwa watu. Huenda hali ikapelekea katika kuadhibiwa, kuuawa na kufedheheshwa. Lakini muda wa kuwa yuko juu ya haki njama za wenye njama hazimdhuru kitu. Endapo atafikwa na yakumfika hapa duniani basi mwisho mwema uko kwake:

وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ

“Mwisho mzuri ni kwa wenye kumcha Allaah.”[2]

[1] 04:69

[2] 07:128

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mujmal ´Aqiydat-is-Salaf as-Swaalih, uk. 05
  • Imechapishwa: 24/05/2022