04. Maneno manne yenye uzito zaidi katika mizani

11 – Juwayriyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka nyumbani kwake mapema asubuhi baada ya kuswali Swalah ya Subh wakati alipokuwa amekaa kwenye msala wake. Wakati kulipopambazuka alikuwa amekaa mahala palepale. Akasema: “Hukutoka katika hali hiyo tangu nilipokuacha?” Akajibu: “Hapana.” Hivyo akasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Nimekariri maneno manne mara tatu baada yako. Lau yangelipimwa pamoja na hayo uliyoyasema basi yangeliyazidi uzito:

سُبْحَانَ الله وَبِحَمْدِهِ عَدَدَ خَلْقِهِ وَرِضَا نَفْسِهِ وَزِنَةَ عَرْشِةِ وَمِدَادَ كَلِمَاتِه

”Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu yote na himdi zote njema ni Zake kwa idadi ya viumbe Wake, radhi Yake, uzito wa ´Arshi Yake na wino wa maneno Yake.”[1]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Hadiyth hii inafahamisha fadhilah za maneno haya manne na kwamba yanalingana na dhikr nyingi sawa na idadi ya viumbe Wake. Ni nani anayedhibiti hesabu yake kama si Allaah pekee?

Hadiyth inathibitisha kuridhia kwa Allaah.

Uzito wa ´Arshi Yake maana yake ni kwamba kwa idadi inayolingana na uzito wa ´Arshi tukufu ambayo ndio dari ya viumbe vyote.

Wino wa maneno Yake maana yake ni mfano wake, kiwango chake na idadi yake:

قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِ مَدَدًا

“Sema: “Endapo bahari ingelikuwa ni wino wa [kuandika] maneno ya Mola wangu, basi ingelimalizika bahari kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu ijapo tungelileta mfano wake kujaza tena.”[2]

[1] Muslim (2726).

[2] 18:109

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 19
  • Imechapishwa: 29/09/2025