04. Hadiyth “Mkishaona mwandamo wa mwezi wa Dhul-Hijjah… ”

Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Mkishaona mwandamo wa mwezi wa Dhul-Hijjah na mmoja wenu akawa na nia ya kuchinja Udhhiyah, basi ajizuilie nywele zake na kucha zake mpaka atakapochinja.” Imekuja katika upokezi mwingine: “Basi asiguse chochote katika nywele zake na ngozi yake.”[1]

Ameipokea Muslim.

Hadiyth hii ni dalili kuwa ikishaingia siku kumi za Dhul-Hijjah na mtu akawa na nia ya kuchinja Udhhiyah, basi asikate chochote katika nywele, kucha wala sehemu yoyote ya ngozi yake hadi atakapochinja Udhhiyah yake. Ikiwa ana wanyama wengi wa Udhhiyah, inajuzu kwake kujikata baada ya kuchinja ya kwanza. Maoni yaliyo wazi zaidi ya wanazuoni ni kuwa hilo ni haramu, kwa sababu msingi wa katazo ni kuonyesha uharamu. Ikiwa mtu atafanya hivyo kwa makusudi, basi anatakiwa atubie na amuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) msamaha. Hakuna fidia juu yake kwa mujibu wa maafikiano. Aidha hilo haliathiri chochote katika Udhhiyah yake.

Katazo hili ni maalum kwa yule mwenye mnyama wa Udhhiyah, hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… na akawa anataka kuchinja…”

Hivyo halimhusu mkewe wala watoto wake ikiwa atataka kuwashirikisha katika thawabu.

[1] Muslim (1977).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 8-9
  • Imechapishwa: 04/05/2025