03. Ni zipi nguzo za imani ya kuamini majina ya Allaah na sifa Zake?

´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 3: Ni zipi nguzo za imani ya kuamini majina ya Allaah na sifa Zake?

Jibu: Ni tatu:

1 – Imani ya kuamini majina mazuri yote.

2 – Imani ya kuamini yale yote ambayo yanaashiriwa na sifa.

3 – Imani ya kuamini hukumu ya sifa na yale mambo yenye kufungamana nazo.

Tunaamini kuwa Allaah ni mjuzi na ana elimu kamilifu iliokizunguka kila kitu.

Tunaamini kuwa Allaah ni muweza na ana uwezo mkubwa kabisa ambao kwao anakiweza kila kitu.

Tunaamini kuwa Allaah ni mwenye huruma na ni mwenye kurehemu na kwamba ana huruma mpana ambao anamrehemu amtakaye.

Hali kadhalika inahusiana na majina mengine yote mazuri na sifa na yale yenye kufungamna nayo.

MAELEZO

 Nguzo za imani ya kuamini majina na sifa za Allaah ni tatu:

1 – Kuamini majina mazuri yote. Inatakiwa kuamini kila jina zuri lililotajwa katika Qur-aan na Sunnah. Kama mfano wa al-´Aliym, al-Hakiym, as-Samiy´ na al-Baswiyr. Allaah ana majina mengi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah ana majina tisini na tisa. Yule mwenye kuyadhibiti ataingia Peponi.”[1]

Hadiyth hii kuna maafikiano juu ya usahihi wake. Ama Hadiyth iliopokelewa na at-Tirmidhiy inayotaja majina hayo tisini na sita, usahihi wake kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) unatakiwa kutazamwa vizuri[2]. Lakini kila jina moja katika majina hayo linaweza kuwa na dalili. Ibn Mandah katika kitabu chake “Kitaab-ut-Tawhiyd” ametaja dalili juu ya majina hayo. Lakini hata hivyo hakuna yeyote anayejua majina yote ya Allaah isipokuwa Yeye Mwenyewe (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nakuomba kwa kila jina ambalo ni Lako ulilojiita Mwenyewe au ukaliteremsha ndani ya Kitabu Chako na ukamfunza mmoja katika viumbe Wako au ukalificha katika elimu iliyofichikana huko Kwako.”[3]

Hii ni dalii inayotuonyesha kuwa majina ya Allaah hayafupiki na kwamba huwafunza baadhi ya waja Wake baadhi ya majina hayo.

2 – Tunaamini zile sifa zilizofahamishwa na majina hayo. Jina al-´Aliym, Mjuzi wa kila jambo, linafahamisha ujuzi. Lakini sifa ya ujuzi wa Allaah ni ujuzi ambao hapitwi na kitu na hakuna chochote kinatoka nje yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَىٰ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا

“Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao, na wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao, na wala chini kuliko ya hivyo na wala wengi zaidi isipokuwa Yeye yupamoja nao popote watakapokuwa.”[4]

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ

“Kwake zipo funguo za mambo yaliyofichikana; hakuna azijuaye isipokuwa Yeye tu.”[5]

Vivyo hivyo jina la al-Qadiyr, Muweza. Tunaamini sifa ya uwezo wa Allaah (´Azza wa Jall) ambao hashindwi na kitu. Kadhalika jina ar-Rahiym, Mwenye kurehemu. Tunaamini sifa ya huruma iliowafunika viumbe wote.

3 – Tunaamini sifa Zake zinazotokana na majina hayo na yaliyofungamana nazo.

[1] al-Bukhaariy (2736) na Muslim (2677).

[2]Dhaifu kwa mujibuwa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf-ul-Jaami´” (1945).

[3] Ahmad (3712), Ibn Hibbaan (972) na at-Twabaraaniy (10352). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (199).

[4] 58:07

[5] 06:59

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 25-27
  • Imechapishwa: 22/09/2021