03. Kumfuata Mtume (صَلَّى ٱللَّٰهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ)

03 – Ufuatiliaji. Ni lazima kuyafuata yale aliyokuja nayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwani hakika matendo hayakubaliwi isipokuwa pale yanapoafikiana na Shari´ah. Hivo ndivo imethibiti katika ”as-Swahiyh” ya Muslim kupitia kwa ´Aaishah:

”Yeyote atakayefanya kitendo kisichokuwa ndani yake amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[1]

Kwa maana kwamba atarudishiwa nayo mwenye nayo.

Kwa hivyo hizi ndio sharti mbili za kukubaliwa matendo yote. Kwa hivyo, ee mwalimu wa kike, hamu yako kubwa isiwe tu kupata mshahara. Bali lifanye lengo lako ni kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kisha kuwanufaisha wasichana wa Kiislamu na kuwaongoza katika kila kheri na kuwatadharisha na kila maovu, khaswa katika zama za leo ambapo zimekithiri fitina na mitihani. Ikiwa uko namna hiyo basi pata bishara njema ya kheri na mafanikio. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Allaah, Malaika wake, watu wa mbinguni na ardhini – hata chungu katika shimo lake na hata nyangumi – wanamswalia ambaye anawafunza watu kheri.”

Ni Hadiyth Swahiyh ambayo ameipokea at-Tirmidhiy.

[1] al-Bukhaariy (13/317) na Muslim (03/1343-1344) nr. 1718.

  • Muhusika: Dr. ´Abdul-´Aziyz bin Daawuud al-Faaiz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tawjiyhaat wa Tanbiyhaat lil-Fataati al-Muslimah, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 27/01/2026