Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah akuogoze katika kumtii – ya kwamba Haniyfiyyah ni dini ya Ibraahiym, nayo ni kumuabudu Allaah peke yake hali ya kuwa ni mwenye kumtakasia Yeye dini. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu.”[1]

Ukishajua kuwa Allaah amekuumba ili umuabudu Yeye, basi jua ya kwamba ´ibaadah haiitwi kuwa ni ´ibaadah, pasi na Tawhiyd. Kama jinsi kuswali hakuitwi kuswali, pasi na wudhuu´. Shirki ikichanganyika na ´ibaadah inabatilika kama jinsi wudhuu´ unavyobatilika unapoingiliwa na hadathi.

Unapojua kuwa shirki inapoingia katika ´ibaadah inaiharibu na kubatilisha kitendo hicho na mwenye nayo anakuwa ni katika wadumishwaji Motoni milele, ndipo utaona kuwa suala hili ni muhimu sana kwa ulazima kulitambua. Huenda Allaah akakusalimisha na mtego huu, jambo ambalo ni kumshirikisha Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema juu yake:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakikaha hasamehi kushirikishwa; lakini anasamehe yasiyokuwa hayo kwa Amtakae.”[2]

Hili litatambulika kwa kuijua misingi mitatu ambayo Allaah (Ta´ala) ameitaja katika Kitabu Chake:

MAELEZO

Mtu akitambua kuwa Tawhiyd inapoingiliwa na shirki inaharibika kama ambavyo wudhuu´ unaharibiwa na hadathi, basi hapo ndio mtu atajua kuwa ni lazima kujua uhakika wa Tawhiyd na shirki ili mtu asitumbukie ndani yake. Matokeo yake Tawhiyd na dini yake vikaharibika. Tawhiyd ndio dini ya Allaah ambayo ni Uislamu na uongofu. Mtu akifanya kitu miongoni mwa aina za shirki, basi Uislamu na dini yake vinabatilika. Kwa mfano mtu awaombe  wafu, awatake uokozi wafu, akaitukana dini, akamtukana Allaah, akamtukana Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamchezea shere na Allaah, Mtume Wake, dini, akaitakidi kuwa ni halali mambo ya haramu ambayo yanatambulika katika dini vyema kuwa ni haramu, kama mfano wa zinaa na mengineyo. Akifanya kitu katika vichenguzi hivi, basi unachenguka Uislamu wake. Ni kama mfano wa anayefanya jambo miongoni mwa mambo yanayochengua wudhuu´, basi wudhuu´ wake unabatilika, kama mfano wa mwenye kutokwa na upepo, kujisaidia haja ndogo au haja kubwa. Katika hali hii wudhuu´ wake unabatilika. Vivyo hivyo ndivyo inavyokuwa juu ya Tawhiyd na Uislamu. Akifanya kichenguzi kimoja miongoni mwa vichenguzi vya Uislamu, basi Tawhiyd na Uislamu wake unabatilika. Anayekanusha uwajibu wa swalah anakufuru. Anayekanusha uharamu wa zinaa anakufuru. Mwenye kuwataka uokozi na kuwawekea nadhiri wafu anakufuru.

Utapojifunza misingi hii ni moja katika mambo yatayokubainishia uhakika wa dini. Misingi hii inapatikana ndani ya Qur-aan. Ukiisoma na kuizingatia, basi mambo yatakubainikia zaidi.

[1] 51:56

[2] 04:116

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 11
  • Imechapishwa: 23/03/2023