9 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Mu´aadh bin Mu´aadh ametuhadithia: Ibn ´Awn ametuhadithia, kutoka kwa al-Ahnaf, ambaye ameeleza kuwa ´Umar amesema:

”Someni kabla hamjakuwa mabwana.”

10 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Muhammad bin Khaazim ametuhadithia: al-A´mash ametuhadithia, kutoka kwa Shaqiyq, kutoka kwa ´Abdullaah, ambaye amesema:

”Naapa kwa Allaah! Ambaye anawatolea watu fatwa katika kila wanachomuuliza ni mwendawazimu.”

al-A´mash amesema:

”al-Hakam akanambia: ”Lau ningelikuwa nimeyasikia maneno haya kutoka kwako hapo kabla, basi nisingelitoa fatwa katika mambo mengi kama nilivofanya.”

11 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Muhammad bin Khaazim ametuhadithia: al-A´mash ametuhadithia, kutoka kwa Rajaa’ al-Answaariy, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Bishr al-Azraq, aliyesema:

”Wakati ambapo Abu Mas´uud al-Answaariy alikuwa amekaa kwenye duara ya kielimu, waliingia wanaume wawili kupitia milango ya Kindah. Akasema mmoja wao: ”Je, si awepo mtu ambaye ataikagua hali yetu?” Bwana mmoja aliyekuweko katika duara ile ya kielimu akasema: ”Mimi.” Ndipo Abu Mas´uud al-Answaariy akachukua kokoto kadhaa kwenye kiganja chake, akawatupia nazo na kumwambia: ”Ilikuwa inachukiza kufanya haraka katika kutoa hukumu.”

12 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Muhammad bin Khaazim ametuhadithia: al-A´mash ametuhadithia, kutoka kwa Swaalih bin Khabbaab[1], kutoka kwa Huswayn bin ´Uqbah, kutoka kwa Salmaan, ambaye amesema:

”Elimu isiyofikishwa ni kama hazina isiyonufaisha.”

13 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Jariyr ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, aliyesimulia: Nimefikiwa na khabari kwamba Mutwarrif bin ´Abdillaah bin ash-Shukhayr amesema:

”Ubora wa elimu ni bora kuliko ubora wa ´ibaadah. Dini yenu iliyo bora ni uchaji.”[2]

14 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Jariyr ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Sulaym, kutoka kwa Hudhayfah, aliyesema:

”Inatosha kuonyesha elimu ya mtu kule kumcha kwake Allaah (´Azza wa Jall). Inatosha kuonyesha uwongo wake kule kusema kwake kuwa anamuomba Allaah msamaha na kutubia Kwake kisha akarejea.”

15 – Abu Khaythamah ametuhadithia: ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa ´Abdullaah bin Murrah, kutoka kwa Masruuq, ambaye amesema:

”Inatosha kuonyesha elimu ya mtu kule kumcha kwake Allaah (´Azza wa Jall). Inatosha kuonyesha uwongo wa mtu kule kujikweza kwake kutokana na elimu yake.”

[1] Imekuja namna katika ile ya asili. Katika maelezo ya nakala nyingine imekuja ”Hayyaan”. Sahihi ni yale tuliyotaja, kama yalivyothibiti vilevile katika nuskha zingine. Ibn Khabbaab ametajwa katika “al-Jarh wat-Ta´diyl” (2/1/499). Isitoshe Ibn Ma´iyn amesema kuwa ni mwenye kuaminika. Cheni yake ni nzuri. Maneno haya yamethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ameyapokea Ahmad na at-Twabaraaniy kupitia njia mbili kutoka kwa Abu Hurayrah. Njia moja wapo ameisimulia mtunzi wa kitabu (162) na Ibn ´Abdil-Barr kupitia kwa Ibn ´Umar.

[2] Yamethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ameyapokea at-Twabaraaniy kupitia kwa Ibn ´Umar na Hudhayfah. Cheni yake ya wapokezi ni nzuri kwa mtazamo wa al-Mundhiriy. al-Haakim ameipokea kupitia kwa Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh). Yeye na adh-Dhahabiy wameisahihisha.

  • Mhusika: Imaam Abu Khaythamah Zuhayr bin Harb an-Nasaa’iy (afk. 234)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-´Ilm, uk. 10-13
  • Imechapishwa: 12/06/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy