Mayahudi walikuwa wakifuata Shari´ah ya Tawraat. Lakini baada ya kufa kwa Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakageuza, wakabadilisha, wakapotosha na wakagawanyika makundi sabini na moja. Wote hao wataingia Motoni isipokuwa tu kundi moja ambao ni wale waliomfuata Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Pindi Allaah alipomtumiliza ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Shari´ah ya Tawraat, akamteremshia Injiyl, akawahalalishia baadhi ya yale waliyoharamishiwa na akawabainishia baadhi ya yale waliyotofautiana, basi mayahudi walimkufuru na wakasema kuwa ni mwana wa uzinzi. Ndipo Allaah akawakadhibisha, akawakufurisha na akateremsha juu yao maneno Yake (Subhaanah):

فَبِمَا نَقْضِهِم مِّيثَاقَهُمْ وَكُفْرِهِم بِآيَاتِ اللَّـهِ وَقَتْلِهِمُ الْأَنبِيَاءَ بِغَيْرِ حَقٍّ وَقَوْلِهِمْ قُلُوبُنَا غُلْفٌ ۚ بَلْ طَبَعَ اللَّـهُ عَلَيْهَا بِكُفْرِهِمْ فَلَا يُؤْمِنُونَ إِلَّا قَلِيلًا وَبِكُفْرِهِمْ وَقَوْلِهِمْ عَلَىٰ مَرْيَمَ بُهْتَانًا عَظِيمًا وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ

“Na kwa kuvunja kwao fungamano lao na kufuru zao kwa Aayah za Allaah na kuua kwao Manabii bila ya haki na maneno ya “Nyoyo zetu zimefumbwa”, bali Allaah amezipiga chapa juu yake kwa sababu ya kufuru zao; basi hawatoamini ila kidogo. Na kwa kufuru zao na kauli yao juu ya Maryam ni usingiziaji mkuu wa kashfa. Na kauli yao: Hakika sisi tumemuua Al-Masiyh ‘Iysaa mwana wa Maryam.”[1]

Vivyo hivyo manaswara baada ya ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupandishwa juu mbinguni walitofautiana juu ya hilo na wakawa makundi sabini na mbili. Wote hao wataingia Motoni isipokuwa tu kundi moja ambao ni wale waliomfuata Muusa, ´Iysaa, Manabii na Mitume wote waliotangulia.

Wakati Allaah alipomtumiliza Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi mayahudi na manaswara wote walimkadhibisha isipokuwa tu wachache katika wao. Matokeo yake wakawa makafiri kwa kitendo cha kumkufurisha Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kupinga ujumbe Wake. Allaah akawasema vibaya na kuwalaumu juu ya kitendo hicho. Aidha akawatishia adhabu na Moto.

Vilevile Allaah amewakufurisha mayahudi kwa kule kusema kwao kwamba al-´Uzayr ni mwana wa Allaah kama ambavo amewakufurisha manaswara kwa kule kusema kwao kwamba Allaah ni al-Masiyh mwana wa Maryam na imani yao kwamba Allaah ni wa tatu wa watatu na kwamba al-Masiyh ni mwana wa Allaah.

[1] 04:155-157

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/articles/78/الاسلام-هو-دين-الله-ليس-له-دين-سواه
  • Imechapishwa: 05/10/2021