1 – Kuzidisha

Pale atakapozidisha mwenye kuswali katika swalah yake kisimamo, kukaa, Rukuu´ au Sujuud kwa kukusudia, basi swalah yake inabatilika. Hata hivyo ikiwa ni kwa kusahau na hakukumbuka kuwa amezidisha ispokuwa mpaka alipomaliza swalah, basi hana juu yake isipokuwa kusujudu Sujuud ya kusahau na swalah yake ni sahihi. Endapo atakumbuka kuwa amezidisha katikati ya swalah, basi itamuwajibikia kwake kurudi mahali hapo na itamuwajibikia kwake kusujudu Sujuud ya kusahau na swalah yake ni sahihi.

Mfano wa hilo:

Mtu ameswali Dhuhr Rak´ah tano na wala hakukumbuka kuwa amezidisha isipokuwa katika Tashahhud. Anatakiwa kukamilisha Tashahhud na kutoa salamu, kisha atasujudu Sujuud ya kusahau kisha atoe salamu. Ikiwa hakukumbuka kuwa amezidisha isipokuwa baada ya kutoa salamu, basi anatakiwa kusujudu Sujuud ya kusahau halafu atoe salamu. Ikiwa atakumbuka kuwa amezidisha katikati ya Rak´ah ya tano, palepale atarudi na kuleta Tashahhud, halafu atatoa salamu kisha atasujudu Sujuud ya kusahau na kutoa salamu.

Dalili ya hilo:

Hadiyth ya ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali Dhuhr Rak´ah tano. Akaambiwa: “Je, kumezidishwa swalah?” Akasema: “Kwa nini?” Wakasema: “Umeswali Rak´ah tano.” Palepale akasujudu sijda mbili baada ya kutoa salamu.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Akainamisha miguu yake na kuielekeza Qiblah na akasujudu sijda mbili kisha akatoa salamu.”[1]

Kutoa salamu kabla ya swalah kumalizika:

Kutoa salamu kabla ya swalah kumalizika huzingatiwa ni katika kuzidisha katika swalah. Mwenye kuswali akitoa salamu kabla ya swalah kumalizika kwa kukusudia, basi swalah yake inabatilika. Ikiwa ni kwa kusahau na asikumbuke hilo isipokuwa baada ya muda mrefu, basi anatakiwa kurudi kuswali upya. Endapo atakumbuka baada ya muda mfupi, kama dakika mbili au tatu, basi anatakiwa kukamilisha swalah yake na kutoa salamu, halafu atasujudu Sujuud ya kusahau kisha atoe salamu.

Dalili ya hilo:

Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalisha Dhuhr au ´Aswr ambapo akatoa salamu baada ya Rak´ah mbili. Kisha akatoka upesi kwenye mlango wa msikiti na huku [Maswahabah] wakisema ya kwamba swalah imefupishwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasimama katika ubao wa msikiti na akaegemea juu yake kama kwamba amekasirika. Akasimama bwana mmoja na kusema: “Je, umesahau au swalah imefupishwa?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Sikusahau na wala swalah haikufupishwa.” Bwana yule akasema: “Ndio, umesahau.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaambia Maswahabah: “Ni kweli ayasemayo?” Wakasema: “Ndio.” Hivyo akatangulia mbele na akaswali zile Rak´ah zilizokuwa zimebaki katika swalah yake halafu akatoa salamu, kisha akasujudu sijda mbili kisha akatoa salamu.”[2]

Imamu akitoa salamu kabla ya swalah yake kumalizika na miongoni mwa maamuma kuko ambao wamepitwa na baadhi ya Rak´ah. Kisha imamu akakumbuka ya kwamba swalah yake ina upungufu, hivyo akasimama kukamilisha zile swalah. Hapo wale maamuma ambao wamesimama ili kulipa zile Rak´ah zilizowapita wana khiyari, ima wataendelea kukidhi zile Rak´ah zilizowapita na watasujudu Sujuud ya kusahau kivyao au wanaweza kurudi na kuungana na imamu na kumfuata. Pindi imamu atakapotoa salamu, basi hao maamuma watalipa zile Rak´ah zilizowapita. Kisha baada ya hapo watasujudu Sujuud ya kusahau baada ya kutoa salamu na hili ndio bora na tahadhari zaidi.

[1] al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, an-Nasaa´iy, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah.

[2] al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sujuud-us-Sahw, uk. 142-144
  • Imechapishwa: 07/04/2022