02. Haki ya Allaah juu ya waja ni kumwabudu na kutomshirikisha na chochote

´Ibaadah ni haki ya Allaah juu ya waja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh):

“Hivi unajua ni haki ipi alonayo Allaah juu ya waja na haki ya waja kwa Allaah? Haki ya Allaah juu ya waja wamwabudu Yeye na wala wasimshirikishe na chochote na haki ya waja kwa Allaah asimuadhibu yule ambaye hakumshirikisha na chochote.”[1]

Hii ndio haki ya kwanza kabisa isiyotanguliwa na chochote na wala isitanguliziwe na haki ya yeyote mwingine. Amesema (Ta´ala):

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee na kuwafanyia wema wazazi wawili.”[2]

قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا

”Sema: “Njooni nikusomeeni yale aliyoyaharamisha Mola wenu kwenu; kwamba msimshirikishe na chochote na muwafanyie wema wazazi wawili… ”[3]

Kutokana na ukubwa wa haki hii, kupewa kwake kipaumbele na kule kuwa ndio msingi ambao hukumu zengine zote za dini zimejengwa juu yake ndio maana tunamuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikaa Makkah miaka kumi na tatu akiwalingania watu kuusimamisha msingi huu na kupinga kumshirikisha. Sehemu kubwa ya Qur-aan imekuja kuuthibitisha na kukanusha shubuha juu yake. Kila mswaliji – ni mamoja swalah ya faradhi au ya sunnah – anamuahidi Allaah kuusimamisha pale anaposema:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“Wewe pekee ndiye tunakuabudu na Wewe pekee ndiye tunakuomba msaada.”[4]

Haki hii kubwa inaitwa Tawhiyd-ul-´Ibaadah, Tawhiyd-ul-Ilaahiyyah au Tawhiyd-ut-Twalab al-Qaswd – yote haya ni majina yenye maana moja. Tawhiyd nii imekita katika maumbile:

“Kila mtoto huzaliwa katika maumbile… “

Upindaji unajitokeza kutokana na malezi mabaya.

“… wazazi wake ndio humfanya akawa mnaswara au akawa mwabudu moto.”[5]

[1] al-Bukhaariy (13/300) na Muslim (30).

[2] 17:23

[3] 06:151

[4] 01:05

[5] Muslim (2047).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 04-05
  • Imechapishwa: 30/07/2018