02. Dhikr inayofuta makosa sawa na povu la bahari

9 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kusema:

سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ

“Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu na himdi zote ni Zake.”

kwa siku mara mia anafutiwa makosa yake hata kama yatakuwa ni mfano wa povu la bahari.”[1]

MAELEZO

Hadiyth inafahamisha fadhilah za dhikr hii:

سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ

“Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu na himdi zote ni Zake.”

na kwamba ni miongoni mwa sababu za kusamehewa. Kusamehewa huku kumewekewa sharti mtu ajiepushe na madhambi makubwa na asiendelee kufanya madhambi madogo. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ

“Mkijiepusha madhambi makubwa mnayokatazwa Tutakufutieni madhambi yenu.”[2]

Dhambi kubwa ni kila ambayo kumepokelewa juu yake kuadhibiwa duniani au matishio huko Aakhirah.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ

“Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu na himdi zote ni Zake.”

Maana ya “na” ni “pamoja” (مع). Kwa maana nyingine ni kwamba unamtakasa Allaah kutokamana na mapungufu pamoja na kumsifu. Amekusanya kati ya kumsifu na kumtakasa. Makusudio ya:

“Mwenye kusema… ”

Aseme hivo kwa kufuatanisha na si kwa kuachanisha mwanzoni mwa mchana au mwishoni mwa usiku. Hakumaanishwi kwamba mtu aseme:

سُبْحَانَ اللَّهِ

“Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu.”

kisha akaishilia hapo, au akasema:

سُبْحَانَ اللَّهِ

“Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu.”

mara kumi kisha akaishilia hapo, ingawa pia analipwa thawabu kwa kufanya hivo.

[1] al-Bukhaariy (6405) na Muslim (2691)

[2] 04:31

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 17
  • Imechapishwa: 28/09/2025