6 – Tambua ya kwamba watu kamwe hawakuzusha Bid´ah isipokuwa waliacha Sunnah mfano wake. Hivyo basi jihadhari na mambo mepya, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah, kila Bid´ah ni upotofu na kila upotofu na watu wake ni Motoni.

7 – Tahadhari na mambo madogomadogo yaliyozuliwa, kwani hakika Bid´ah ndogondogo hupea mpaka zikawa kubwa. Kila Bid´ah iliyozushwa katika ummah huu mwanzo wake ilikuwa ndogo na inafanana na haki. Hivyo akadanganyika yule aliyetumbukia ndani yake na matokeo yake hakuweza kutoka ndani yake. Ikapea na ikawa ni dini ambayo mtu anaamini kuwa ni dini. Hatimaye mtu akaenda kinyume na Njia iliyonyooka na akatoka katika Uislamu.

8 – Zingatia – Allaah akurehemu – kila ambaye utasikia maneno yake miongoni mwa watu wa zama zako, usifanye haraka na wala usijiingize katika chochote katika hayo mpaka kwanza uulize na uchunguze: Je, kuna yeyote katika Maswahabah zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyelizungumza au yeyote katika wanazuoni? Ukipata masimulizi yoyote kutoka kwao, basi shikamana nayo. Usiyavuke kwa ajili ya kitu kingine, na usikipe kipaumbele kitu kingine badala yake ukaja kutumbukia Motoni.

9 – Tambua kupinda kutoka katika Njia iliyonyooka ni kwa namna mbili. Wa kwanza ni mtu ameteleza akapinda kuiacha Njia, pamoja na kuwa hakukusudia isipokuwa kheri. Kosa lake lisichukuliwe kama kiigizo, kwa sababu ni mwenye kuangamia.

Mwengine ameifanyia ukaidi haki na akaenda kinyume na wale wachaji waliokuwa kabla yake. Huyo ni mpotevu, mwenye kupotosha wengine na ni shaytwaan aliyeasi katika ummah huu. Yule mwenye kumfahamu ni lazima kwake kutahadharisha naye na kuwabainishia watu hali yake ili asije yeyote akatumbukia katika Bid´ah yake na hivyo akaangamia.

10 – Tambua – Allaah akurehemu – ya kwamba hautatimia Uislamu wa mja mpaka awe ni mwenye kufuata, mwenye kusadikisha na mwenye kujisalimisha. Yule mwenye kudai ya kwamba kuna jambo lolote katika Uislamu ambalo hawakututosheleza nalo Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi amewakadhibisha. Hilo litatosha kuwa ni kujitenga nao na amewatukana. Ni mzushi, mpotevu na mwenye kuwapotosha wengine na mwenye kuzusha ndani ya Uislamu yasiyokuwemo.

  • Mhusika: Imaam Abu Muhammad al-Hasan bin Khalaf al-Barbahaariy (kfk. 329)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh-us-Sunnah, uk. 68-70
  • Imechapishwa: 11/12/2024