Kuna ambao wameyakanusha majina na sifa za Allaah, kama vile Jahmiyyah. Wengine wamekanusha sifa Zake, kama vile Mu´tazilah. Wote hawa wawili ni Mu´attwilah.

Wengine wamezipindisha maana pale waliposhindwa kuzikanusha dalili zenyewe au kukanusha maana zake. Hawa ni Mu´awwilah.

Wengine wakaziona kuwa ni katika maandiko ambayo maana yake haiko wazi ambayo hakuna yeyote anayejua tafsiri yake isipokuwa Allaah pekee. Wanaona kuwa tunatakiwa kuyasoma maandiko na tusiyafasiri kwa sababu ni miongoni mwa maandiko yasiyokuwa wazi. Hawa ni Mufawwidhwah.

Baadhi ya wengine wakapindukia katika kuzithibitisha sifa za Allaah na wakazifananisha na sifa za viumbe. Hawa ni Mumaththilah na Mushabbihah.

Kuhusu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, wamethibitisha maandiko na maana yake vile ambavyo imefahamisha Qur-aan na Sunnah. Kwa msemo mwingine hawakuyapotosha, hawakuyapindisha maana wala hawakusema kuwa ni katika maandiko yasiyokuwa wazi. Ahl-us-Sunnah wanaona kuwa maandiko yanayozungumzia sifa za Allaah yako wazi yanayotambulika kwa njia ya kwamba inatambulika maana yake. Hata hivyo namna yake haitambuliki. Sio katika yale maandiko ambayo hayako wazi kwa njia ya kwamba haitambuliki maana yake. Maana yake iko wazi. Aidha Ahl-us-Sunnah wanasema kuwa sifa za Allaah hazifanani na sifa za viumbe na kwamba zinalingana na Yeye pekee. Hii ndio ´Aqiydah waliokuwa nayo Maswahabah, wanafunzi wa Maswahabah na wale waliowafuata kwa wema ambao wanafuata mfumo huu. Mfumo huu maana yake ni kuzithibitisha sifa za Allaah kama zilivyokuja pasi na kuzifanyia namna, kuzikengeusha, kuzifananisha wala kuzilinganisha. Zinathibitishwa kama zilivyokuja kwa njia inayolingana na Allaah (´Azza wa Jall). Si kama sifa za viumbe:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ وَهُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah daima na maimamu wao, kuanzia Maswahabah, wale waliowafata kwa wema, wale waliokuja baada yao na wakapita juu yao.

[1] 42:11

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 23/07/2024