Himdi zote njema zinamstahikia Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa kutatokea mgawanyiko katika ummah huu kama ilivyotokea katika nyumati zilizotangulia. Pindi yatatokea hayo akatuusia kushikamana barabara na yale aliyokuwa akifuata yeye (Swalla Allaahu ´alyhi wa sallam) na Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ´anhum). Amesema (Swalla Allaahu ´alyhi wa sallam):

“Mayahudi wamegawanyika katika mapote sabini na moja, manaswara wakagawanyika katika mapote sabini na mbili na ummah wangu utagawanyika mapote sabini na tatu. Yote hayo yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Kukaulizwa: “Ni kina nani, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni lile litakalofuata yale ninayofuata mimi hii leo na Maswahabah zangu.”[1]

“Hakika yule miongoni mwenu atakayeishi umri mrefu basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na ziumeni kwa magego. Tahadharini na mambo ya kuzua! Hakika kila kitachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[2]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… na kila upotevu ni Motoni.”[3]

Namna hii ndivyo katuusia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kushikamana na yale aliyokuwa akifuata yeye na Maswahabah wake wakati pindi kutatokea migawanyiko.

[1] at-Tirmidhiy (2641) na wengineo. Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Hadiyth ni Swahiyh na inayojulikana katika ”as-Sunan” na ”al-Masaanid”.” (Majmuu´-ul-Fataawaa (03/345)).

Ni Hadiyth Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh al-Jaamiy´ as-Swaghiyr” (01/245), ”as-Swahiyhah” (03/480), ”Dhwilaal-ul-Jannah fiy Takhriyj-is-Sunnah” (09, 31, 35), ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud (03/869), ”Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (2/334) na ”Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (02/364).

[2] Ahmad (04/126,127), Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676), Ibn Maajah (42), (43), (44), ad-Daarimiy (96) na wengineo. Imaam at-Tirmidhiy amesema:

”Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh.”

al-Haakim amesema:

”Hadiyth hii ni Swahiyh na haina kasoro.” (al-Mustadrak (01/96)

Haafidhw Ibn Kathiyr amesema baada ya kunakili maneno ya al-Haakim:

”Ameisahihisha pia Haafidhw Abu Nu´aym al-Aswfahaaniy na ad-Daghawliy. Shaykh-ul-Islaam al-Answaariy amesema:

”Ndio Hadiyth bora na nzuri zaidi kwa  watu wa Shaam.” (Tuhfat-ut-Twaalib, uk. 163)

´Allaamah al-Albaaniy amesema:

”Ni Swahiyh.” ”Irwaa´ (08/107-109)

[3] an-Nasaa´iy (1578), Khuzaymah (1785) na al-Bayhaqiy (279). Shayk-ul-Islaam amesema:

”Ameipokea an-Nasaa´iy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Ameongeza:

”Kila Bid´ah ni upotofu.”

´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akitoa Khutbah kwa maneno haya.” (Iqaamat-ud-Daliyl ´alaa Ibtwaal-it-Tahliyl, uk. 58)

´Allaamah al-Albaaniy amesema:

”Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh kama alivosema Shaykhl-ul-Islaam Ibn Taymiyyah.” (Khutbat-ul-Haajah, uk. 26)

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: as-Salafiyyah haqiyqatuhaa wa simaatuhaa, uk. 05-13
  • Imechapishwa: 06/05/2024