Swawm katika lugha ina maana ya kujizuia kabisa. Kwa mfano mtu anapokaa kimya huitwa kuwa ameswawm. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Maryam:

إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا

“Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa rehema ya kujizuia [na kusema], hivyo basi leo sitomsemesha mtu yeyote.”[1]

Kwa maana kwamba nimejizuilia maneno.

Waarabu pia husema kwamba farasi ameswawm pale ambapo anakuwa amejizuilia kula na kufanya kazi.

Lakini swawm katika Shari´ah mwajibikaji kujizuilia kwa kuweka nia kutokana na vifunguzi kuanzia kuchomoza kwa alfajiri ya pili mpaka jua linapozama[2]. Makusudio ya kujizuilia ni muislamu kujiepusha na vifunguzi vyote. Makusudio ya kuweka nia ni uazimie na kukusudia jambo hilo kwa moyo wako usiku kabla ya alfajiri kwamba unafunga kuanzia alfajiri mpaka kuzama kwa jua. Ikiwa muislamu atafunga bila nia, basi swawm yake haisihi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hakika si vyenginevyo matendo yanalipwa kutegemea nia.”

[1] 19:26

[2] al-Mughniy (3/105), at-Ta´riyfaat (136) na ”Fath-ul-Baariy” (04/102).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr Dhil-In´am bisharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/431-432)
  • Imechapishwa: 13/02/2025