1 – Abu Khaythamah Zuhayr bin Harb ametuhadithia: Wakiy´ ametuhadithia: al-A´mash ametuhadithia, kutoka kwa Tamiym bin Salamah, kutoka kwa Abu ´Ubaydah, aliyesimulia kuwa ´Abdullaah amesema:

”Kuwa mwanachuoni au mwanafunzi, wala msikue kitu kingine kati ya hayo mawili.”

2 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Ishaaq bin Sulaymaan ar-Raaziy ametuhadithia: Nimemsikia Handhwalah amesimulia kuwa ´Awn bin ´Abdillaah, ambaye amesema:

”Nilimwambia ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz: ”Inasemekana ukiweza kuwa mwanachuoni basi uwe mwanachuoni. Usipoweza, basi uwe mwanafunzi. Usipoweza kuwa mwanafunzi, basi wapende. Usipowapenda, basi usiwachukie.” ´Umar akasema: ”Allaah ametakasika kutokana na mapungufu! Kwa hakika Allaah (Ta´ala) amemjaalia njia ya kutokea.”

3 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Jariyr ametueleza, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Tamiym bin Salamah, kutoka kwa Abu ´Ubaydah, aliyesimulia kuwa ´Abdullaah amesema:

”Yule ambaye Allaah anamtakia kheri, basi humpa ufahamu akaielewa dini.”[1]

4 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Mu´aawiyah bin ´Amr ametuhadithia: Zaa-idah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Tamiym bin Salamah, kutoka kwa Abu ´Ubaydah, aliyeeleza kuwa ´Abdullaah amesema:

”Enyi watu! Jifunzeni! Na yule mwenye kujifunza basi afanyie kazi.”

5 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Sufyaan bin ´Uyaynah ametuhadithia, kutoka kwa ´Aaswim bin Abiyn-Najuud, kutoka kwa Zirr bin Hubaysh, ambaye amesema:

”Nilimwendea Swafwaan bin ´Assaal al-Muraadhiy, ambaye akasema: ”Ni kipi kilichokuleta?” Akasema: ”Kujifunza elimu.” Ndipo akasema: ”Hakika Malaika huziteremsha mbawa zao juu ya mwanafunzi hali ya kuridhia kile anachokitafuta[2].”

6 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Muhammad bin Khaazim ametuhadithia: al-A´mash ametuhadithia, kutoka kwa Shimr, kutoka kwa Sa´iyd bin Jubayr, kutoka kwa Ibn ´Abbaas, aliyesema:

”Hakika yule ambaye anawafunza watu kheri anaombewa msamaha na kila kiumbe mpaka na nyangumi baharini.”[3]

7 – Abu Khaythamah ametuhadithia: ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy ametuhadithia: Bishr bin Mansuur ametuhadithia, kutoka kwa Thawr, kutoka kwa ´Abdul-´Aziyz bin Dhwabyaan, aliyeeleza kuwa al-Masiyh, mwana wa Maryam, amesema:

”Atakayejifunza, akafunza na kutendea kazi, huyo ni mtukufu mbinguni.”

8 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Muhammad bin Khaazim ametuhadithia: al-A´mash ametuhadithia, kutoka kwa Shaqiyq, kutoka kwa ´Abdullaah, ambaye amesema:

”Jifunzeni! Kwani hakika mmoja wenu hajui ni lini atahitajia.”[4]

[1] Haya yamesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ameyapokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Mu´aawiyah (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] Katika nuskha zingine imekuja ”… kwa yale anayotafuta”.  Imekuja namna hiyo ikiwa ni pamoja na at-Tirmidhiy na ameisahihisha. Baadhi ya wasimulizi wameisimulia kama maneno ya Swahabah na wengine wameisimulia kama maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hali yoyote, yana hukumu sawa na maneno ya kinabii, kwa sababu jambo kama hilo halisemwi kutokana na vile mtu anavyojionea, kama alivosema Ibn ´Abdil-Barr katika “Jaamiy´ Bayaan-il-´Ilm wa Fadhwlih” (1/32-33).

[3] Maneno hayohayo yamesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ameyapokea at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Awsatw” kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) na at-Tirmidhiy, ambaye ameisahihisha, kupitia kwa Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ´anh).

[4] Bi maana pindi watu watapohitaji elimu yake.

  • Mhusika: Imaam Abu Khaythamah Zuhayr bin Harb an-Nasaa’iy (afk. 234)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-´Ilm, uk. 8-10
  • Imechapishwa: 12/06/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy