Lengo la kwanza: Kuihakikisha Tawhiyd

Miongoni mwa malengo makubwa na matukufu zaidi ya hajj ni kuihakikisha Tawhiyd kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) na kujitenga mbali na kinyume chake ambacho ni kumshirikisha Allaah. Hili ni kusudio na lengo kubwa zaidi. Kwa sababu Tawhiyd ndio msingi ambao Allaah (´Azza wa Jall) ametuumba kwa ajili yake na ili tuihakikishe.

Kupitia ´ibaadah, desturi tukufu na nembo za hajj zilizobarikiwa inapata kudhiri nafasi kubwa ilionayo Tawhiyd, manzilah yake ya juu na kwamba ndio msingi ambao dini ya Allaah (´Azza wa Jall) inajengwa juu yake; kunajengwa juu yake kila tendo jema ambalo muumini anajikurubisha kwalo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Bali kila tendo jema na ´ibaadah ambayo haikusimama juu ya Tawhiyd ya Allaah na kujiweka mbali na shirki, Allaah haikubali kutoka kwa yule mtendaji. Kwa ajili hii Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) kama ilivyotajwa katika ”as-Swahiyh” ya Muslim katika mazingira yake wakati alipohiji pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatangaza Tawhiyd hali ya kusema: ”Nimekuitikia, ee Allaah, nimekuitikia, huna mshirika Wewe, nimekuitikia. Hakika himdi zote, neema na ufalme vyote ni Vyako. Hakika huna mshirika Wewe.”[1]

Maneno haya matukufu ni maneno ya Tawhiyd, kumtakasia nia Allaah (Jalla wa ´Alaa) na ni kujitenga mbali na shirki. Upande mwingine washirikina walikuwa wakitangaza shirki na kumfanyia Allaah washirika. Katika ”as-Swahiyh” ya Muslim amepokea kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza:

”Washirikina walikuwa wakisema: ”Nimekuitikia, huna mshirika… ” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anafika anawaambia:  ”Ole wenu! Tosha! Tosha” halafu wanasema: ”… isipokuwa mshirika ambaye ni Wako unammiliki na anachokimiliki.” Wanayasema haya pamoja na kuwa wanatufu kwenye Nyumba.”[2]

Katika maneno yake ”huna mshirika Wewe” ambayo yamekuja katika Talbiyah mara mbili; mara ya kwanza pale alipomuitikia kwa kusema: ”Nimekuitikia, ee Allaah… ” na mara ya pili pale aliposema ”Hakika himdi, neema na ufalme vyote ni Vyako.” Mara ya kwanza inajumuisha kwamba hana mshirika katika kuitikia wito huu. Mara ya pili inajumuisha kwamba hana mshirika katika sifa zote kamilifu, neema na ufalme. Ikishathibiti ya kwamba sifa zote kamilifu ni za Allaah, neema zote ni zenye kutoka kwa Allaah na ufalme wote ni Wake na hana mshirika katika yote hayo kwa njia yoyote ile, hivyo basi apwekeshwe peke yake katika Talbiyah, kumnyenyekea, kumpenda, kujisalimisha na kumtii. Vipi mtu atamfanyia Allaah mshirika katika ´ibaadah ambaye hamiliki katika ulimwengu huu hata kijiwavu cha kokwa ya tende, isitoshe hama pamoja na Allaah ushirika katika ufalme, hamiliki manufaa wala kuzuia madhara, hakuna mikononi mwake kupeana wala kukizuia kitu? Ametakasika Allaah kutokamana na yale yote wanayomshirikisha. Bali jambo lote ni la Allaah ambaye hana mshirika. Hii ni dalili ya waziwazi kabisa inayothibitisha ubatilifu wa shirki na kwamba washirikina ndio watu wapumbavu, wapotevu na viumbe waliopotea zaidi kutoka katika njia iliyonyooka. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Miyqaat wakati alipotangaza hajj:

“Ee Allaah! Hakika hii ni hajj na hakuna kujionyesha ndani yake wala kutaka kusikika.”[3]

Kisha akaenda Makkah hali ya kuwa ni mwenye kuleta Talbiyah kwa maneno ya Tawhiyd matukufu ambayo ndani yake kuna Tawhiyd na kuihakikisha na  wakati huohuo kujiweka mbali na yale yaliyo kinyume nayo. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiyarudirudi katika njia yake ya kuelekea Makkah na katika kuhamahama kwake katika nembo mbalimbali za hajj.

Halafu kule kutufu kwenye Nyumba, Sa´y kati ya Swafaa na Marwah, kusimama ´Arafah, kusimama Muzdalifah na kutekeleza matendo ya hajj mengine, yote hayo ndani yake kuna utiifu na ´ibaadah mbalimbali ambazo zimesimama juu ya Tawhiyd. Ni wajibu kwa mahujaji wote kwa matendo na utiifu wote wakusudie uso wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwani hakika Allaah hakubali matendo ya mtendaji yeyote isipokuwa tu pale ambapo yatakuwa yamejengwa juu ya kumpwekesha Yeye pekee (´Azza wa Jall). Kwa ajili hii imekuja katika Hadiyth al-Qudsiy:

“Hakika Mimi nimejitosheleza kabisa kutokamana na shirki. Hivyo basi, yule atakayetenda tendo akanishirikisha Mimi pamoja na mwingine, basi Nitamwacha yeye na shirki yake.”[4]

Ni wajibu kwa yule mtamkaji ambaye Allaah (´Azza wa Jall) amemkirimu kuleta Talbiyah kwa maneno haya matukufu ahudhurishe ndani ya moyo wake maana yake, aelewe yanafahamisha nini na ajitahidi maisha yake yote awe ni mwenye kuhakikisha Tawhiyd ambayo imefahamishwa nayo. Hivyo anakuwa ni mwenye kumtakasia ´ibaadah Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa njia ya kwamba hamwombi mwingine isipokuwa Allaah, hamtaki uokozi mwingine asiyekuwa Allaah, hamtegemei asiyekuwa Allaah, hachinji isipokuwa kwa ajili ya Allaah, haweki nadhiri isipokuwa kwa Allaah na wala hatekelezi aina yoyote ile ya ´ibaadah isipokuwa tu kumfanyia Allaah pekee:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ

“Sema: “Hakika swalah yangu na vichinjwa vyangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu.” Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa.”[5]

kwa njia ya kwamba anakuwa ni mwenye kushikamana barabara na Tawhiyd, mwenye kuipiga vita shirki, mwenye kuijali na kuchunga haki zake. Sambamba na hilo anajiepushe na vile vitenguzi vyake na yale yanayopingana nayo katika kumshirikisha Allaah na huku anakuwa ni mwenye kuchukua tahadhari kwelikweli ya kutumbukia ndani yake, katika kitu chochote kinachoisababisha au njia inayopelekea kwayo. Maisha yake yote yanakuwa juu ya haya, kufa kwake kunakuwa juu ya haya na atafufuliwa juu ya haya kwa idhini ya Allaah (´Azza wa Jall).

[1] Muslim (1218).

[2] Muslim (1185).

[3] Ibn Maajah (2890). Katika cheni ya wapokezi wake kuna udhaifu. Shaykh al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) ameitaja katika ”Silsilat-us-Swahiyhah” (2617) yanayoisapoti na hivyo inapata kuwa nzuri (Hasan) kupitia zengine.

[4] Muslim (2985).

[5] 06:162-163

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 05-10
  • Imechapishwa: 10/08/2018