01. Imani ni maneno na matendo, inazidi na inapungua

Abu Muhammad ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Haatim amesema:

“Nilimuuliza baba yangu na Abu Zur´ah kuhusu madhehebu ya Ahl-us-Sunnah katika misingi ya dini na madhehebu waliowakuta nayo wanachuoni ulimwenguni kote na ambayo wao wawili wanaitakidi juu ya hilo. Wakasema:

“Tulikutana na wanachuoni Hijaaz, ´Iraaq, Shaam na Yemen na madhehebu yao ilikuwa:

1- Imani ni maneno na matendo, inazidi na inapungua.”

MAELEZO

Hii ni ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambayo Ibn Abiy Haatim alimuuliza baba yake na Abu Zur´ah. Kama kawaida yake alikuwa akiwauliza kuhusu Hadiyth, kasoro zake na wapokezi, kwa sababu walikuwa ni majibali inapokuja katika elimu, kuhifadhi na ´Aqiydah ya dini na Shari´ah. Kwa ajili hiyo ndio maana al-Laalakaa´iy ameitilia umuhimu na akaiandika ndani ya kitabu chake “Sharh Usuul I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah” kama ambavyo vilevile alitilia umuhimu Kitabu cha Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) “Usuul-us-Sunnah”. Allaah amrehemu na amjaze kheri.

Ibn Abiy Haatim amesema:

“Nilimuuliza baba yangu na Abu Zur´ah kuhusu madhehebu ya Ahl-us-Sunnah katika misingi ya dini na madhehebu waliowakuta nayo wanachuoni ulimwenguni kote na ambayo wao wawili wanaitakidi juu ya hilo.”

Jambo la kwanza ameuliza kuhusu misingi ya dini. Jambo la pili amewauliza wamewakuta wanachuoni wakiitakidi nini. Ni ipi ´Aqiydah yao? Ni upi mfumo wao? Waliwakuta wanachuoni ulimwenguni kote wakionelea nini? Wao wenyewe wawili wanaitakidi nini? Amewauliza kuhusu ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah, ´Aqiydah ya wanachuoni wa ulimwenguni na ´Aqiydah yao wao wawili. Wakajibu:

“Tulikutana na wanachuoni Hijaaz, ´Iraaq, Shaam na Yemen na madhehebu yao ilikuwa:

1- Imani ni maneno na matendo, inazidi na inapungua.”

Hivi ndivyo walivyokuwa wakiitakidi wanachuoni ulimwenguni kote. Kabla yao Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) na wale wenye kuwafuata kwa wema waliitakidi hivo, ya kwamba imani ni maneno na matendo na inazidi kwa matendo mema na inapungua kwa maasi. Haya yanathibitishwa na Qur-aan na Sunnah tofauti na wanavyoonelea Murji-ah na Khawaarij.

Aina ya kwanza ya Murji-ah wanaonelea kuwa imani ni utambuzi wa moyo tu. Hii ni ´Aqiydah ya Jahmiyyah. Ni I´tiqaad ya kikafiri. Ndio ´Aqiydah ya Ibliys. Ibliys anamtambua Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) na baadhi ya sifa Zake (Subhaanahu wa Ta´ala) na kwamba Yeye ndiye Muumba Aliye na nguvu na ukamilifu na kwamba Yeye ndiye anamwongoza amtakaye na anampoteza amtakaye:

قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ ۖ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ

“Akasema: “Kutokana na ulivyonihukumia kupotoka, nitawakalia katika njia Yako iliyonyooka. Kisha nitawaendea mbele yao na nyuma na kuliani kwao na kushotoni kwao na wala hutopata wengi wao ni wenye kushukuru.” 07:16-17

Anatambua uola wa Allaah na nguvu Zake na kuwa Yeye ndiye anamwongoza na kumpoteza amtakaye.

Jahmiyyah hawa kama tulivyosema wanaonelea kuwa imani ni utambuzi tu. Hawa ndio Jahmiyyah waliyopindukia.

Aina nyingine ya Murji-ah ni wale wanaoitwa “Murji-ah al-Fuqahaa´”, wanachuoni Murji-ah. Wanaonelea kuwa imani ni maneno ya ulimi na kusadikisha kwa moyo na wanaondosha matendo.

Khawaarij wanaonelea kuwa imani ni maneno, matendo na kuamini lakini haizidi na wala haipungui. Wanaonelea kuwa imani ni kitu kimoja tu ambacho hakizidi na wala hakipungui.

Ahl-us-Sunnah wao wanaitakidi kuwa imani imo moyoni, mdomoni na kwenye viungo vya mwili na kwamba ni kuitakidi kwa moyo, kutamka kwa ulimi na matendo ya viungo vya mwili.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qurrat-ul-´Aynayn bi Tawdhwiyh Ma´aaniy ´Aqiydat-ir-Raaziyayn, uk. 03-07
  • Imechapishwa: 09/10/2016