Tunamshukuru Allaah kwa yale aliyotupa ilhamu kwayo. Tunamuomba Allaah atuwafikishe kuyatendea kazi kwa vitendo yale tuliyoyajua. Kwani hakika kheri haifikiwi isipokuwa kwa tawfiyq na msaada Wake. Yule mwenye kuongozwa na Allaah, basi hakuna wa kumpotosha katika viumbe Wake. Swalah na amani zimwendee Muhammad, bwana wa viumbe wote, kwa ndugu zake katika Mitume na Manabii na wale watakaofuata na kwa wale watakaofuata nuru ambayo imeteremshwa pamoja naye mpaka siku ya Qiyaamah.

Hakiki mimi nakuusia, ee mwanafunzi, kutakasa nia katika kutafuta kwako elimu na kupambana kuitendea kazi kwa vitendo. Elimu ni mti na matendo ni matunda. Mtu hazingatiwi kuwa mwanachuoni pale ambapo haitendei kazi elimu yake. Imesemekana kuwa elimu ni baba na matendo ni mtoto. Matendo yanakuwa pamoja na elimu na uelewa unakuwa pamoja na masimulizi. Kwa hivyo usijihisi raha kwa matendo muda wa kuwa huna raha na elimu. Wala usijihisi raha kwa elimu muda wa kuwa ni mwenye kufanya mapungufu katika matendo yako. Hata hivyo kusanya kati ya hayo mawili ingawa yatakuwa machache. Hakuna kitu dhaifu kama elimu ya mwanachuoni iliyoachwa na watu kutokana na njia yake mbaya na ujinga wa mjinga uliochukuliwa na watu kwa sababu ya kuangalia ´ibaadah yake. Ikiwa Allaah atatunuku kutokana rehema Zake na akamtimizia neema Yake juu ya mja Wake, humpa kiasi kidogo cha yote mawili ambacho kikaokoa huko Aakhirah. Ama kujihami na kupuuza, kupenda urahisi na kubweteka, kupendelea upunguzaji na ulaini na kumili katika raha na faraja, yanapelekea katika mambo yenye kuchukiza na matokeo yake ni mabaya.

Malengo ya elimu ni matendo, malengo ya matendo ni uokozi. Ikiwa matendo hayasheheni elimu, basi elimu ya mwanachuoni huyo huwa ni majuto. Tunamuomba Allaah atukinge na elimu inayompeleka mtu kwenye majuto, ikapelekea katika utwevu na ikawa ni mzigo juu ya mabega ya mwanachuoni huyo. Wamesema baadhi ya wenye hekima:

”Elimu inahudumia matendo na matendo ndio malengo ya elimu. Ingelikuwa sio kwa sababu ya kutenda, basi asingelikuweko yeyote mwenye kutafuta elimu. Na ingelikuwa sio kwa sababu ya elimu, basi kusingelifanywa matendo yoyote. Inapendeza zaidi kwangu kuacha haki kutokana na kutoijua kuliko kuiacha kwa sababu ya kuichukia.”

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr Ahmad bin ´Aliy al-Khatwiyb al-Baghdaadiy (afk. 463)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Iqtidhwaa’-ul-´Ilm al-´Amal, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 06/05/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy