Himdi zote njema anastahiki Allaah, Aliye hai, Mwenye kuwasimamia viumbe wote, Mmoja, wa Pekee, Ambaye anakusudiwa na viumbe wote, Ambaye kila mmoja anamtegemea. Ambaye hakuzaa wala hakuzaliwa, na hakuna yeyote anayelingana Naye.

Himdi zote njema anastahiki Allaah, ambaye hakujifanyia mwana na hana mshirika katika ufalme na wala hakuwa dhalili mpaka awe anahitaji mlinzi.

Himdi zote njema anastahiki Allaah, Aliye juu kabisa, Mtukufu, Ambaye hakuna chochote kilicho mfano wake, Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona, Ambaye sifa Zake kuu zinatofautiana na sifa za viumbe hata zitakuwa na majina ya kushirikiana.

Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye daima ni Mwenye ni kusifiwa kwa sifa Zake kuu, Anayeitwa kwa majina Yake mazuri mno. Utakasifu ni wa Mola wako, Mola wa nguvu asiyeshindika, kutokana na yale wanayoyaeleza na pia kutokana na yale wanayoyasema wale wanaofananisha na kukanusha. Amri na uumbaji ni Wake. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu!

Swalah na amani zimwendee bwana wetu Muhammad, Nabii asiyekuwa msomi, kizazi chake na Maswahabah zake mpaka siku ya Qiyaamah.

Naandika – Allaah akitaka – ndani ya kitabu hiki Hadiyth arobaini kuhusu sifa za Allaah (´Azza wa Jall), zikiambatana na baadhi ya nukuu muhimu kutoka kwa Salaf. Allaah ndiye Mwenye kuwafikisha katika yale anayoyapenda na kuyaridhia. Hapana matikiso wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 28/05/2024