Jambo lililotukusanya ni kama mlivyosikia kutoka kwa Shaykh Swaalih (Waffaqahu Allaah) ”Asbaab sa´aadat-il-Usrah”. Ni jambo lenye umuhimu mkubwa. Sote tuko na familia, wadogo wetu na wakubwa wetu. Sote tunatumai kuona furaha nyumbani. Kila mmoja anatamani kuona furaha usoni mwa mke na watoto wake. Sote tunatamani kupata furaha.

Hapana shaka kuwa familia ndio msingi wa jamii. Familia ikiwa ni yenye furaha na yenye utulivu, basi jamii inakuwa ni yenye utulivu na yenye furaha.

Ni wajibu kwetu kujua pindi tunapozungumzia furaha ya familia hatukusudii familia isiwe na matatizo yoyote. Miongoni mwa maumbile pindi watu wanapokusanyika ni kutokea baadhi ya kasoro na baadhi ya matatizo. Tunacholenga ni msingi wa familia uwe na furaha na raha na familia iweze kuwa na uwezo wa kukabiliana na matatizo kwa njia ambayo haitoondosha ile furaha na raha yake. Tunalenga furaha ijae kwenye familia kwa njia ya kwamba baba akiingia nyumbani furaha iangaze katika familia na pindi anapotoka familia yake inasubiri kurejea kwake. Kwa msemo mwingine tunachotaka kulenga ni kwamba mume ahisi raha kwa mke wake, mke ahisi raha kwa mume wake, wavulana wahisi raha kwa baba yao na wazazi wahisi raha kwa watoto wao na raha itaendea katika majumba.

Ni jambo lenye kujulikana kuwa familia ni yenye kujengwa juu ya msingi na matawi. Msingi wake ni mume na mke na matawi yake ni yale matunda ya ndoa; watoto wakiume na wakike. Ni jambo lenye kujulikana furaha ikipatikana kuanzia katika msingi basi itatambaa mpaka kwa watoto.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Asbaab sa´aadat-il-Usrah, uk. 13
  • Imechapishwa: 08/10/2016