01. Funga ya ambaye amelala mchana akatokwa na manii

Swali: Akiota mfungaji mchana wa Ramadhaan swawm yake inaharibika? Ni lazima kwake kuharakisha kuoga?

Jibu: Kuota hakuharibi funga. Kwa sababu mfungaji hakufanya hivo kwa kutaka kwake mwenyewe. Ni lazima kwake kuoga josho la janaba pindi atakapoona manii.

Akiota baada ya swalah ya fajr na akachelewesha kuoga mpaka wakati wa swalah ya dhuhr ni sawa. Vivyo hivyo hakuna neno kwake akimjamii mke wake wakati wa usiku na asiwahi kuoga isipokuwa baada ya kuchomoza kwa alfajiri. Kwani imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alikuwa akiamka akiwa ni mwenye janaba inayotokana na jimaa kisha anaoga na kufunga. Vivyo hivyo hakuna neno kwa mwenye hedhi na mwenye damu ya uzazi iwapo watasafika wakati wa usiku na wasioge isipokuwa baada ya kuchomoza alfajiri. Swawm zao ni sahihi. Hata hivo haijuzu kwao wawili hawa wala kwa aliye na janaba kuchelewesha kuoga au wakachelewesha swalah mpaka jua likachomoza. Bali ni lazima kwa wote hao kufanya haraka kuoga kabla ya kuchomoza kwa jua ili wapate kuswali ndani ya wakati. Ni lazima kwa mwanamme kuharakisha kuoga josho la janaba kabla ya swalah ya fajr ili aweze kutekeleza swalah katika mkusanyiko.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ashyaa´ laa tufsid-is-Swawm, uk. 03-04
  • Imechapishwa: 27/03/2021