01. Dibaji ya “Ujuwb-ul-´Amal bis-Sunnah”

Himdi zote anastahiki Allaah. Mwisho mwema ni wa wachaji Allaah. Swalah na salaam zimwendee mja na Mtume Wake, Mtume wetu Muhammad aliyetumwa akiwa ni rehema kwa walimwengu na hoja kwa waja wote, kizazi chake, Maswahabah wake ambao walikibeba Kitabu cha Mola Wao (Subhanaah) na Sunnah za Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waliokuja baada yao kwa uaminifu wa hali ya juu na kuvihifadhi kikamilifu sawa maana na matamshi yavyo – Allaah awawie radhi na atujaalie kuwa miongoni mwa wenye kuwafuata kwa wema.

Amma ba´d:

Wanachuoni wameafikiana tangu hapo kale na sasa ya kwamba misingi yenye kuzingatiwa katika kuthibitisha hukumu na kubainisha ya halali na haramu ni Kitabu cha Allaah kitukufu kisichoingiliwa na batili kutoka kwa mbele yake wala kwa nyuma yake, kisha Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye hatamki kwa matamanio yake na hayakuwa ayasemayo isipokuwa ni Wahy wenye kuteremshwa halafu maafikiano ya wanachuoni wa Ummah. Hata hivyo wanachuoni wakatofautiana juu ya misingi mingine ambapo muhimu zaidi katika misingi hiyo ni kipimo (Qiyaas). Wanachuoni wengi wanaonelea kuwa ni hoja pale itapotimiza masharti yake yenye kuzingatiwa. Dalili juu ya misingi hii ni nyingi sana zisizohesabika wala kudhibitiwa.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ujuwb-ul-´Amal bis-Sunnah
  • Imechapishwa: 23/10/2016